Habari

Mutyambai azima polisi waliozoea hongo katika vizuizi barabarani

June 19th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai Jumatano ameamuru kuondolewa kwa vizuizi na vituo vya ukaguzi wa magari katika barabara kuu kote nchini.

Vizuizi na vituo vya ukaguzi sasa vitawekwa tu kwa idhini ya makamanda wa polisi katika ngazi ya kaunti na sharti viwekwe kwa sababu maalum.

Bw Mutyambai alisema makamanda wa polisi watawajibishwa kwa mienendo mibaya ya maafisa wa polisi chini ya usimamizi yao, mathalan upokeaji wa rushwa.

“Mabadiliko haya tayari yanaendelea kama yanavyoweza kuthibitishwa na idadi ya vizuizi vilivyoko katika barabara kutoka Mombasa hadi Malaba.

“Tunatoa wito kwa Wakenya wenye nia njema kutuunga mkono kwa kutii sheria na kujiepusha na vitendo vya ufisadi,” akasema kwenye taaarifa iliyotumiwa kwa vyombo vya habari Jumatano na afisi yake.

Bw Mutyambai alisema udumishaji wa usalama barabarani ni mojawapo ya masuala ambayo ameyapa kipaumbele.

“Ili kufikia lengo hilo pande husika, wenye magari na polisi, wanapasa kujiepusha na vitendo vya ufisadi na vile vile waripoti visa hivyo kwa asasi husika,” akaeleza.

Hatua hii ya Bw Mutyambai inamaanisha kuwa maafisa wa polisi ambao watahudumu katika barabara kuu watafanya hivyo chini ya amri ya kamanda wa polisi katika maeneo husika kwa sababu maalum.

Tayari baadhi ya makamanda wameamuru kwamba vizuizi vya barabarani viondolewe.

“Maafisa walio ndani ya miji watashauriwa kuhakikisha hamna msongamano wa magari. Na wale walioko nje ya miji waondoke mara moja na wasubiri kushughulikia ajali ambayo yanapaswa kushughulikiwa mara moja huku tukisubiti maagizo zaidi kutika afisa za juu,” akasema barua iliyoandikiwa na kamanda mmoja kwa wadogo wake.

Alipoingia afisini, Bw Mutyambai aliahisi kulainisha idara ya polisi wa trafiki nchini kama sehemu ya mchakato wa kupambana ufisadi katika sekta hiyo.

Kumekuwa na malalamishi kuwa maafisa wa polisi wa trafiki, haswa wale barabara kuu ni wafisadi mno.

Maafisa wote wasimamizi wa vituo (OCS) pia waliamriwa kuhakikisha kuwa sheria za usalama barabarani almaarufu sheria za Michuki, zinatekelezwa.

Juzi, Naibu Inspekta Jenerali Edward Mbugua alisema kuwa operesheni zote za trafiki zimegatuliwa hadi kiwango cha kituoni ili kuhakikisha zinafanikiwa.