Kimataifa

Muuaji aliye pia mbakaji aomba korti impe hukumu ya kunyongwa

June 7th, 2024 1 min read

NA MASHIRIKA

RAIA wa Afrika Kusini, Thabo Bester, aliyepatikana na hatia ya ubakaji na mauaji, alishangaza Mahakama Kuu ya Free State, alipoomba apewe adhabu ya kifo (Hukumu ya kifo) juu yake.

Nchini Afrika Kusini, adhabu ya kifo ilikomeshwa mwaka wa 1995 ingawa mahakama kwa kiasi kikubwa ziliepuka kutoa hukumu hiyo kuanzia 1990 huku kukiwa na nia ya kumaliza utawala wa ubaguzi wa rangi.

Ombi la Bester, halikuishia hapo, mhalifu huyo pia alitaka kuachiliwa kwa washtakiwa wenzake, wanaokabiliwa na mashtaka yanayohusiana na kutoroka gerezani.

Bester anayejulikana kama Facebook Rapist katika mtandao wa kijamii, anakabiliwa na shtaka la kujifanya wakala ambaye aliwasaidia wasichana kupata kazi kwenye televisheni.

“Ninahisi sio haki kwa watu hawa ambao wameketi hapa kama washtakiwa wenzangu kuwa mahakamani wakati najua vizuri kwamba hawana uhusiano wowote na hili,” alieleza Bester.

“Mheshimiwa, ninasema hivi kama mtu aliyevunjika moyo, na nasema hivi kwa moyo wote; inanivunja moyo sana kuwaona watu hawa katika mahakama hii. Nikijua wazi kwamba wanateseka kwa jambo ambalo hawajui lolote kulihusu,” aliendelea Bester.

Mshtakiwa huyo tayari anakabiliwa na kifungo cha maisha jela kwa makosa yake ya zamani.

Alifika mahakamani bila uwakilishi wa kisheria baada ya mawakili wake wa hivi punde kujiondoa kutokana na mzozo ulioripotiwa kuhusu ada.

Mahakama ilimpa siku saba kupata wakili mpya. Mhalifu alipatikana na hatia, pamoja na mpenziwe Bi Nandipha Magudumana na wengine saba.

Walikuwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi Mei 2022 kuhusiana na kutoroka kwake katika gereza la Mangaung.

Bw Bester, Bi Magudumana na dereva Zanda Moyo watabaki gerezani, washtakiwa wengine saba waliachiliwa kwa dhamani ya Sh68,950.