Kimataifa

Muuguzi afutwa kazi kwa kumpa mgonjwa wa kansa Biblia

May 28th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

UINGEREZA

MAHAKAMA moja iliamua kuwa hatua ya kumfuta kazi mhudumu wa afya ambaye alijaribu kumpa mgonjwa wa saratani Biblia ilifaa.

Muuguzi huyo wa Uingereza kwa jina Sarah Kuteh alifutwa kazi katika hospitali ya Darent Valley, eneo la Dartford mnamo 2016 kwa kuzungumza na wagonjwa kadha kuhusu imani yake kwa Yesu na hata akajitolea kuwapa Biblia.

Mlalamishi katika kesi alieleza korti kuwa wakati mmoja wa wagonjwa kusema kuwa alikuwa na uhuru wa kimawazo kuhusu dini, Kuteh alieleza kuwa “njia ya pekee ya kumpokea Mungu ilikuwa kupitia kwa Yesu.”

“Alimwambia kuwa angempa Biblia ikiwa hakuwa nayo, akashika mkono wake na kuomba maombi yaliyotisha kwa muda, kisha akamtaka kuimba wimbo wa kitabu cha Zaburi 23. Mgonjwa aligundua kuwa waliimba pamoja na mhudumu huyo kifungu cha kwanza,” sehemu ya uamuzi wa korti ikasema.

Aidha, nakala za korti zilionyesha kuwa muuguzi huyo alimwambia mgonjwa huyo kuwa endapo angemwomba Mungu, alikuwa na nafasi nzuri ya kupona ugonjwa huo.

Matukio hayo yanasemekana kusababisha kufutwa kwake kazi, kwa makosa makubwa.

Baada ya uamuzi huo wa korti, Kuteh ambaye ni mama wa watoto watatu alijaribu kukata rufaa akisema korti “ilikosa kuzingatia maadili ya kufanya kazi ya wauguzi na kutofautisha maelezo yanayofaa na yasiyofaa kuhusu imani za kidini.”

Aidha, alisema kuwa jopokazi ya kuamua kuhusu kesi yake ilikosa kuzingatia kuwa ana haki za kidini.

Lakini wiki iliyopita, majaji wa mahakama ya rufaa walitupa rufaa yake, wakisema “hospitali haikuwakataza wafanyakazi wake kushiriki haki za kidini kazini.”

“Kilichoonekana kuwa kisichofaa ni kwa mlalamishi (Kuteh) kuanzisha mazungumzo kuhusu dini na kukosa kutii maagizo ya wasimamizi wa kazi,” majaji wakasema.

Majaji hao walielewana kuwa jopokazi iliyoamua kumfuta kazi ilikuwa sawa, na kuwa haikuvunja haki zake.

Imetafsiriwa na Peter Mburu