Dondoo

Muumini apokonya kanisa viti

August 16th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KAEWA, MASINGA

KIOJA kilishuhudiwa katika kanisa moja la hapa muumini mmoja alipoamua kubeba viti alivyokuwa amenunulia kanisa baada ya kuzozana na pasta.

Duru zinasema jamaa alikuwa rafiki wa karibu wa pasta huyo lakini wakaanza kuzozana, hali iliyofanya muumini huyo kugura kanisa hilo.

“Haikujulikana walikosania nini kwa sababu wawili hao walikuwa marafiki wakubwa tangu pasta alipoanza kuhudumu hapa miaka miwili iliyopita, ” alisema mdokezi.

Siku ya kioja jamaa huyo alifika kanisani na kuanza kuvuruga pasta akimwambia ameharibu kanisa.

“Mimi binafsi sikutaki hapa. Umekuwa dikteta wa kupindukia na ninakuomba uende zako. Tutatafuta pasta mwingine wa kutuhubiria. Uongozi wako umekuwa wa kutilia shaka na tangu ulipokuja hapa mipango yetu ya kanisa imeanza kurudi nyuma,” jamaa alimwambia pasta.

Pasta huyo alijitetea vikali akimlaumu jamaa kwa kuwa na tamaa lakini kalameni huyo alisimama kidete na kumtaka pasta aondoke.

“Kinachokuwasha ni nini? Kwa nini unaniita dikteta. Umepandwa na pepo la tamaa? Siendi mahali popote, wewe peke yako hautanifanya niondoke hapa,” pasta alimjibu jamaa.

Inasemekana jamaa alikasirika na kuchukua baadhi ya viti akidai ndiye aliyevinunua.

“Kama umekataa kuondoka nitaenda na mali yangu. Viti hivi ni mimi niliyenunua na sitaviacha,” jamaa alisema.

Inasemekana waumini wengine walitazama sinema hiyo huku wengine wakinong’onezana kuhusu tukio hilo. Jamaa alikusanya viti alivyodai vilikuwa vyake na kwenda zake.

Watu walioshuhudia kioja hicho waliangua vicheko walipomuona jamaa huyo akibeba viti hivyo kwa pikipiki yake. Hata hivyo haikujulikana kilichojiri baada ya kioja hicho.