Habari MsetoSiasa

Muungano mkuu Jubilee, ODM na KANU wanukia

June 28th, 2019 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG

CHAMA tawala cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Orange Democratic Movement (ODM) chake kiongozi wa upinzani Raila Odinga, vinapanga muungano wa kisiasa ambao utafanikishwa kwenye kura ya maamuzi.

Duru ndani ya vyama hivyo zilifahamisha Taifa Leo kwamba, vyama vya Kenya African National Union (Kanu) kinachoongozwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi na Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi vimekuwa vikishiriki mazungumzo ya siri kwa lengo la kuunda muungano huo.

Inasemekana kuwa chama cha Wiper cha aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka na vyama vingine vidogo vinaweza kushirikishwa huku wanaounga kura ya maamuzi wakilenga kuunganisha nchi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Ingawa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakisisitiza kuwa muafaka wao hauhusu uchaguzi mkuu wa 2022, wadadisi wanasema kutokana na mazungumzo ya siri ambayo yamekuwa yakiendelea, muungano wao hauwezi kuepukika.

Mnamo Aprili, Rais Kenyatta alimtetea Bw Odinga wafuasi wa Naibu Rais William Ruto walipomlaumu kwa kupanga kuvunja chama cha Jubilee.

Alisema mazungumzo yake na Bw Odinga yalilenga kuimarisha maisha ya Wakenya na hayakuwa ya kisiasa.

“Raila hajaniambia kwamba anataka kuwa Rais 2022 na mimi sijamuambia ninataka kuendelea kuwa Rais 2022. Tumekuwa tukijadili masuala yanayoathiri watu wetu,” Rais Kenyatta alisema.

Bw Odinga pia amekuwa akisisitiza kuwa muafaka wake na Rais Kenyatta ulikuwa wa kuunganisha Wakenya.

Hata hivyo, mnamo Machi, Seneta wa Siaya, James Orengo, mmoja wa washirika wakuu wa Bw Odinga, alifichua kwamba ODM kimezungumza na Rais Kenyatta kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022, madai ambayo mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi alikanusha.

Lakini licha ya Rais na Bw Odinga kukanusha, duru za karibu na viongozi hao zinasema kuna mipango ya Jubilee, ODM, Kanu, ANC, Wiper na vyama vingine kuungana.

“Muungano huo utajitokeza kwenye kampeni za kura ya maamuzi na Wakenya wanaweza kushuhudia muungano mkubwa zaidi wa kisiasa jinsi ODM kilivyobuniwa baada ya kura ya maamuzi ya 2005,” duru ziliambia Taifa Leo.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna (pichani), Alhamisi alisema hana habari kuna mazungumzo ya kuunda muungano lakini akaongeza kuwa chama kilikuwa na mkutano kujadili mfumo wa kuunda miungano siku zijazo.

“Tutajadili miungano iliyopita na jinsi ilivyoathiri matokeo pamoja na mfumo wa kuwa na miungano siku zijazo, ni sehemu ya tutakayojadili kwenye mkutano wa baraza kuu la chama,” alisema.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju alisema kuwa manifesto ya chama hicho ni ya kuunganisha Wakenya wote. “Manifesto ya Jubilee ni kuunganisha Wakenya wote. Sio baadhi yao, lakini wote bila ubaguzi,” alisema Bw Tuju.

Naye Katibu Mkuu wa Kanu, Nick Salat alisema muungano huo unawezekana.

“Muungano unaweza kuwepo. Kinachounganisha vyama hivi ni suala la kura ya maamuzi. Ni muhimu kuhakikisha kura ya maamuzi inafanyika bila vurugu,” alisema Bw Salat.