Muungano wa Azimio wakosa meno ya ‘kuuma’

Muungano wa Azimio wakosa meno ya ‘kuuma’

CHARLES WASONGA Na BENSON MATHEKA

MUUNGANO wa Azimio la Umoja One Kenya unaonekana kukosa makali ya kukosoa mipango na ajenda za Serikali ya Kenya Kwanza (KKA) ndani na nje ya bunge licha ya kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Ingawa muungano huo unasema utatekeleza jukumu lake la kukosoa serikali, wadadisi wanasema kuna kila dalili kwamba hauna kucha za kufanya hivyo kwa kuzidiwa na weledi wa Rais William Ruto na muungano wake wa Kenya Kwanza.

“Wabunge wa Azimio hawaonekani kuwa na ari hasa baada ya Dkt Ruto kuvamia baadhi ya vyama tanzu vya muungano huo na kuongeza idadi ya wabunge walio upande wake,” akasema mdadisi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Anasema japo vinara wa muungano huo wanaweza kuwa na nia ya kukosa serikali, wabunge, kama majemedari wao wanaonekana kukosa makali.

Na hali inaweza kuwa mbaya zaidi baada ya mieizi mitatu ambayo vyama tanzu vitafunguliwa kujiondoa kulingana na mkataba wa muungano huo.

Kulingana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, jumla ya wabunge 173 walichaguliwa kwa tiketi za vyama tanzu ndani ya Azimio ilhali wabunge 164 walichaguliwa kwa tiketi ya vyama vya vilivyoko Kenya Kwanza. Wabunge wengine 12, walichaguliwa kwa tiketi huru.

Lakini baada ya Rais William Ruto kutangazwa mshindi katika kinyang’anyiro cha urais mnamo Agosti 15, alianzisha kampeni ya kuvutia baadhi ya wabunge wa Azimio upande wa KKA.

Kufuatia hatua hiyo wabunge saba wa chama cha United Democratic Movement (UDM), wabunge watatu wa KANU, wabunge watatu wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) na wawili waliochaguliwa kwa tiketi ya Maendeleo Chap Chap (MCC) walijiunga walijiunga na mrengo huo unaoongozwa na Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema kuwa Azimio imekosa nguvu na makali ya kutoa jasho mrengo wa serikali ndani ya nje ya bunge kutokana na mgawanyiko miongoni mwa wabunge na maseneta wake.

“Hii ilidhihirika katika matokeo ya uchaguzi wa uspika katika bunge la kitaifa na seneti. Bw Moses Wetang’ula alishinda kwa jumla ya kura 215 huku mwaniaji wa Azimio Kenyatta Kenneth Marende alipata kura 130 pekee. Hii inaashiria wabunge kadha wa Azimio walipiga kura pamoja na Kenya Kwanza,” wakili Mark Oloo alisema baada ya uchaguzi huo.

Utovu wa umoja ndani ya Azimio pia ulidhihirika mapema wiki hii pale wabunge watano pekee ndio walijitokeza kushiriki maandamano yaliyoitishwa na muungano huo jijini, Nairobi.

Maandamano hayo yaliitishwa kupinga kusimamishwa kazi kwa naibu Afisa Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ruth Kulundu.

Wafuasi wa Azimio walisusia maandamano hayo katika makao makuu ya tume hiyo katika jumba la Anniversary Towers, Nairobi, yaliyoongozwa na Mbunge wa Ruaraka T.J Kajwang’ na mwenzake wa Makadara George Aladwa.

Hii ndio maana, maandamano hao yalitibuliwa haraka na maafisa wa polisi waliowatawanya wabunge hao kwa kuwarushia vitoa machozi.

Katika ishara ya kukosa pumzi, jana ni wabunge wasiozidi 20 wa Azimio walihudhuria kikao na wanahabari kilichoongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka jijini Nairobi kukosoa hotuba ambayo Rais Ruto alitoa bungeni Alhamisi.

“Nawahimiza wabunge wetu wa Azimio kuanzisha uchunguzi kuhusu mpango wa utoaji mbolea kwa bei nafuu. Tunahoji jinsi mbolea hiyo ilinunuliwa, mahala ambako ilinunuliwa na kiwango cha pesa za umma zilizotumiwa kuinunua,” Bw Musyoka akasema.

Walioandamana naye ni pamoja na; kiongozi wa mrengo wa Azimio katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi, Esther Passaris (Mbunge Mwakilishi wa Kike, Nairobi), Makali Mulu (Kitui Mashariki), Sarah Korere (Laikipia Kaskazini), John Mbadi (Mbunge Maalum), miongoni mwa wengine.

Na licha ya baadhi ya wabunge hao wa Azimio kuapa kuangusha baadhi ya mawaziri wateule 22 waliopendekezwa na Rais Ruto Jumanne wiki hii, dalili zinaonyesha juhudi zitaambulia patupu.

“Ukweli ni kwamba licha ya idadi kubwa ya wabunge kuchaguliwa kwa tiketi ya vyama vya Azimio, hawataweza kuvuruga uteuzi wa mawazri wateule wenye dosari za kimaadili. Hii ni kwa sababu hawana mshikamo miongoni mwao. Wengine wameanza kujipendekeza kwa serikali ilivyodhihirika baada ya kuapishwa kwa Rais Ruto,” Bw Javas Bigambo alisema juzi kwenye mahojiano kwenye runinga moja ya humu nchini.

  • Tags

You can share this post!

Ruto aunda jopokazi la wasomi kuchunguza CBC

DARUBINI YA WIKI: TOLEO NAMBARI 5, Oktoba 02, 2022

T L