Habari

Muungano wa maendeleo ya wanawake walaani ghasia za Murang’a

October 6th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MUUNGANO wa Maendeleo ya Wanawake Nchini (MYWO) umelaani vikali ghasia zilizotokea wikendi eneo la Kennol, Murang’a.

Mapigano hayo yaliyohusisha kundi la ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’, yalisababisha vifo vya watu wawili wakati wa ziara ya Naibu wa Rais William Ruto eneo hilo ambapo alihudhuria hafla ya Kanisa la AIPCA.

Dkt Ruto alizuru Murang’a mnamo Jumapili ambapo aliongoza hafla ya kuchangisha pesa za kanisa baada ya kuhudhuria ibada ya misa.

Mwenyekiti wa MYWO, Rahab Mwikali amesema Jumanne kwamba matukio ya kisiasa yanayoendelea kushuhudiwa nchini yanatia muungano huo wasiwasi.

Rahab alisema mgawanyiko unaoonekana kati ya wanasiasa na viongozi serikalini, ni tishio kwa amani na umoja wa taifa.

“Kama muungano wa wanawake, tunahuzunishwa na matukio ya kisiasa tunayoona. Ni muhimu viongozi na wanasiasa wafahamu watoto wangali nyumbani na wanatazama yanayoendelea,” amesema mwenyekiti huyo wa MYWO, huku akilaani vikali ghasia za Murang’a.

Mkurupuko wa Covid-19 nchini, ulisababisha shule kufungwa mnamo Machi 2020, hivyo basi wanafunzi wanaendelea kusalia nyumbani.

Kufuatia maafa ya vijana wawili, Peter Mbothu, 15, na Christopher Kariuki, 21, eneo la Kenol, Rahab amesema ghasia zinapoibuka wanaoathrika zaidi ni kina mama, watoto na vijana.

“Tunahimiza viongozi wa kidini wasiruhusu wanasiasa kufanya kampeni kanisani,” amesema, akieleza kusikitishwa na hali ya sasa ambapo maeneo ya kidini yamegeuzwa uga wa siasa na kampeni.

Akahimiza: “Wahubiri warejeshe taswira ya kitambo ya maeneo ya kuabudu kulisha wafuasi chakula cha kiroho.”

Aidha, muungano huo unahimiza Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto wasuluhishe tofauti zinaoonekana kuibuka kati yao, ili kuondoa au kutuliza joto la kisiasa.