HabariSiasa

Muungano wa Ruto na Kalonzo wang'oa nanga

December 8th, 2019 2 min read

Na KITAVI MUTUA

Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Bw Musyoka ataungana na Dkt Ruto, hasa wakati huu ambapo ameachana na Bw Odinga. Hili ni kwa kuwa Bw Musyoka hawezi kushinda urais bila kubuni muungano wa kisiasa – Victor Munyaka, mbunge wa Machakos Mjini

SIKU chache baada ya tetesi kuibuka kuwa Naibu Rais William Ruto “anamtongoza’ makamu wa rais wa zamani, Bw Kalonzo Musyoka, kwa dhamira ya kuunda muungano, kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2022, sasa imeanza kuibuka wazi kuwa mchakato wa kuunda ushirikiano huo umeng’oa nanga.

Mpango huo ulianza kujisuka bayana pale wandani wa Dkt Ruto kutoka eneo la Ukambani walipozidisha kasi za kubuni muungano baina yake na kiongozi wa Wiper, Bw Musyoka kabla ya 2022.

Taifa Jumapili imebaini kwamba washirika wa viongozi hao wawili wamekuwa wakikutana kujadili uwezekano wa kushirikiana kisiasa kwenye uchaguzi wa 2022.

Hata hivyo, hakuna mkakati uliopitishwa kufikia sasa. Mashauriano kati ya pande hizo mbili yanajiri baada ya chama cha ODM kutangaza kuwa kimekomesha ushirikiano wake na Wiper.

Vyama hivyo vimeshikiriana kisiasa kwa karibu miaka kumi iliyopita

Inaaminika kuwa mashauriano hayo yamechangiwa na hatua ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kuanza ushirikiano mpya na magavana Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni) kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw Musyoka.

Bw Musyoka alikuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga kwenye chaguzi za urais za 2013 na 2017.Majuzi, Katibu Mkuu wa ODM Bw Edwin Sifuna alitangaza kwamba ushiriano kati ya vyama hivyo viwili uliisha rasmi baada ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra.

Alisema kuwa Dkt Mutua ndiye mshirika wao mpya wa kisiasa katika eneo hilo. Dkt Mutua anaongoza chama cha Maendeleo Chap Chap.

Mjadala kuhusu muungano huo ulishika kasi wiki hii, baada ya aliyekuwa Seneta wa Machakos Bw Johnstone Muthama kuwaalika wabunge wa Ukambani wanaoegemea upande wa Dkt Ruto nyumbani kwake, ambapo pendekezo hilo lilijadiliwa kwa kina.

Wabunge waliofika ni Victor Munyaka (Machakos Mjini), Vincent Musyoka (Mwala), Nimrod Mbai (Kitui Mashariki) na Fabian Muli (Kangundo).

Wabunge hao wamekuwa wakipigia debe muungano huo.Kulingana na Bw Munyaka, mazungumzo hayo yanalenga kubuni muungano kati ya Bw Musyoka na Dkt Ruto, kama vile Rais Kenyatta anavyoshirikiana kisiasa na Bw Odinga.

Bw Munyaka alithibitisha kwamba wamekuwa wakikutana na wabunge wenzao na kuwa uongozi wa Wiper umekumbatia pendekezo la kubuni ushirikiano wa kisiasa na vyama vingine.

Kambi ya Dkt Ruto inatumaini kwamba kwa kumfikia Bw Musyoka, itapanua ushirikiano wake kisiasa, ili kuimarisha nafasi yake kuwania urais mnamo 2022.

“Kwanza, tunataka kumaliza uhasama wetu wa kisiasa na wenzetu kutoka Wiper ili kuanzisha mazungumzo muhimu kuhusu mwelekeo wa kisiasa ambao utaifaa jamii yetu,” alisema mbunge huyo kwenye mahojiano.

Alisema kwamba hilo litaleta jamii hiyo pamoja, hali ambayo itaiwezesha kuzungumza kwa sauti moja kisiasa.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Bw Musyoka ataungana na Dkt Ruto, hasa wakati huu ambapo ameachana na Bw Odinga. Hili ni kwa kuwa Bw Musyoka hawezi kushinda urais bila kubuni muungano wa kisiasa,” akasema.

Haikubainika kama Bw Muthama alikuwa ameshauriwa na Bw Musyoka kujadili mpango huo. Bw Musyoka na washirika wake hawajakanusha kuwepo kwa mazungumzo hayo.

Kauli ya Bw Munyaka iliungwa mkono na Bw Musyoka (Mwala) na Bw Mbai (Kitui Mashariki) kwenye mahojiano tofauti na kituo cha redio cha Musyi FM.

Wabunge hao walisema kuwa baada ya kusambaratika kwa muungano wa NASA, imefikia wakati Bw Musyoka abuni muungano wa kisiasa na Dkt Ruto.