Habari

Muungano wa Ruto na Raila ni ndoto – Kositany

July 1st, 2020 2 min read

Na ONYANGO K’ONYANGO

WANDANI wa Naibu wa Rais William Ruto, wamepuuzilia mbali uwezekano wa kufanya muungano wa kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Caleb Kositany, alisema Bw Odinga ataharibu mipango yao ya 2022 iwapo ataungana na Naibu wa Rais.

Mbunge huyo wa Soy, alisema kuwa Naibu wa Rais ana ufuasi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya na wakazi wa eneo hilo watamwacha endapo ataungana na Bw Odinga.

“Tukiungana na Bw Odinga tutapoteza uungwaji mkono katika eneo Mlima Kenya. Rais Uhuru Kenyatta anakumbana na upinzani mkubwa katika eneo la Mlima Kenya kwa sababu ya ushirikiano wake na Bw Odinga. Dkt Ruto hawezi kufanya makosa hayo, akasema Bw Kositany.

“Tuko tayari kuungana na mwanaisasa yeyote, wakiwemo Mudavadi na Wetang’ula, isipokuwa Raila,” akaeleza.

Mbunge wa Belgut Nelson Koech na mwenzake wa Keiyo Kusini Daniel Rono pia walipuuzilia mbali juhudi za mbunge wa Emurrua Dikir Johanna Ngeno kujaribu kuwaunganisha Bw Odinga na Dkt Ruto kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Wawili hao walisema kuwa Naibu wa Rais anaungwa mkono na idadi kubwa ya watu katika maeneo ya Magharibi na Mlima Kenya hivyo, Bw Odinga hatakuwa wa manufaa kwake endapo wataungana.

Bw Koech alisema kwamba Bw Odinga anaweza kusababisha wanasiasa wanaounga mkono Dkt Ruto kumtoroka.

Mbunge huyo anayehudumu kwa muhula wa kwanza, hata hivyo, alikiri kuwa Bw Odinga alihusika katika kumnoa kisiasa Dkt Ruto.

Naye Bw Rono, alisema Dkt Ruto yuko tayari kushindana na Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

“Suala la kuwapatanisha Naibu wa Rais na Raila ni sawa na ndoto ya mchana. Raila hawezi kumsaidia Dkt Ruto kushinda urais,” akasema Bw Rono.

“Sisi tutaungana na Bw Mudavadi na Wetang’ula; wao pia waungane na wasimamishe Raila na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka tukutane kwa debe 2022,” akasema.

Naibu wa Rais na Bw Odinga wamekuwa mahasimu wa kisiasa tangu Dkt Ruto alipogura chama cha ODM kabla ya uchaguzi wa 2013.

Tangu Rais Uhuru Kenyatta alipoungana na Bw Odinga miaka 2018, Dkt Ruto na kiongozi wa ODM wamekuwa wakirushiana cheche za maneno. Wadadisi wanasema kuwa uhasama wa kisiasa baina ya wawili hao unasababishwa na siasa za 2022.

Lakini kulingana na Bw Ngeno, baadhi ya wazee kutoka Bonde la Ufa wameelezea nia ya kutaka kuwapatanisha Dkt Ruto na Bw Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mbunge huyo wa Kanu alisema inawezekana kwa Bw Odinga kufanya kazi pamoja na Dkt Ruto na kutikisa ulingo wa kisiasa kama ilivyokuwa 2007.

Nazo duru katika kambi ya Dkt Ruto zimedokezea Taifa Leo kwamba kumekuwa na shinikizo za kumtaka Naibu wa Rais kushirikiana kisiasa na Bw Odinga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.