Habari

Muungano wa vijana dhidi ya ukeketaji waanza kuibadilisha sura ya Isiolo

February 7th, 2020 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

[email protected]

BAADA ya ngoja ngoja hatimaye vijana wa Kaunti ya Isiolo wana kila sababu ya kutabasamu hasa kuhusiana na masuala ya ukeketaji.

Hii ni kufuatia uzinduzi rasmi wa tawi la Kaunti ya Isiolo la muungano wa vijana dhidi ya ukeketaji (Youth Anti-FGM Network). Haya yalifanyika katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupambana na ukeketaji, sherehe iliyoandaliwa katika uwanja wa Police Grounds, Kaunti ya Isiolo.

Katika hafla hiyo, muungano wa vijana dhidi ya ukeketaji nchini, Youth anti-FGM Network – Kenya, ulitoa rasmi mawasilisho mbele ya serikali ambapo mojawapo ya maombi yao ni kuwakilishwa katika bodi ya kitaifa ya kupambana na ukeketaji.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhazili Mkuu Msimamizi – Waziri Msaidizi – katika Wizara ya Utumishi wa Umma na Jinsia Bi Rachel Shebesh alisema kwamba huku kipindi cha kuhudumu cha bodi hiyo kikikaribia kuisha, serikali itajitahidi kuhakikisha kwamba vijana wanaoendesha kampeni dhidi ya ukeketaji watahusishwa.

“Bodi ijayo itakapoundwa tutahakikisha kwamba kuna mwakilishi wa vijana,” alisema Bi Shebesh.

Wanachama wa tawi hili jipya wamepewa dhamana na jukumu la kuunganisha vijana na kuendesha kampeni dhidi ya ukeketaji katika kaunti ya Isiolo.

Kwa sasa, Isiolo inaorodheshwa miongoni mwa kaunti zilizo na idadi kubwa ya visa vya ukeketaji nchini.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mwakilishi wa Hazina ya Umoja wa Mataifa inayohusika na idadi ya watu – UNFPA nchini Dkt Ademola Olajide na Bi Agnes Pareiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Kupambana na ukeketaji.