Habari Mseto

Muungano wa wafanyabiashara wasikitikia wanaotegemea wateja wa baa

March 19th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI 

MISAKO dhidi ya baa zinazohudumu siku nzima imelemaza mfumo kuendeleza uchumi kwa muda wa saa 24 mfululizo eneo la Mlima Kenya.  

Hii ni kwa mujibu wa mwenyekiti wa muungano wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Bw Alfred Wanyoike, akisema huduma za baa zimethibitisha kuchangia kuimarika kwa sekta mbalimbali za biashara.

Akiongea Mjini Thika, Bw Wanyoike alisema shughuli za kibiashara ambazo baa hushirikisha ni pamoja na wachuuzi wa bidhaa za kula na kunywa, mavazi na vitu vya jumla, huku maduka mengi yanayohudumu usiku yakisalia kufungwa kwa sababu ya amri kali ya oparesheni dhidi ya pombe haramu na hatari.

Aidha, alilalamikia sekta ya uchukuzi kuathirika nayo ikiwa imeunganishwa na vituo vya kuuza petroli, kwa sababu ya amri hiyo.

“Mfumo wa kukuza uchumi saa 24 unatishiwa, ikizingatiwa kuwa mwenye baa huajiri maweita na mabaunsa wanaochangia kulipa ushuru,” akasema.

Isitoshe, mwenyekiti huyo wa muungano wa wafanyabiashara eneo la Kati alitaja wachuuzi wa bidhaa rejareja, kama vile njugu na kripsi kwenye baa na vituo vya burudani kukosa kukosa unga kwa sababu ya amri inayoweza kutekelezwa ipasavyo.

Bw Wanyoike anapendekeza kuwe na utathmini mpya wa kuendesha vita hivyo vya ulevi kiholela, akisema kupigana na biashara halali ni sawa na kupigia debe umaskini.

“Hata ingawa tunaunga mkono misako hiyo ya pombe za mauti na mihadarati, serikali ni kama haielewi kwamba pombe hizo hazitengenezewi ndani ya baa. Mihadarati pia haiuzwi ndani ya baa,” akasema.

Bw Wanyoike alisema kwamba kufunga baa kwa msingi wa vita dhidi ya pombe za mauti ni sawa na kuua mtoto kwa msingi kwamba amezaliwa na mama mlemavu.

“Baa ni mtoto wa watengenezaji pombe. Serikali izingatie msako wake kwa watengenezaji wa pombe za mauti. Bila pombe za mauti sokoni na bila kukubaliwa kuwe na uchukuzi wa pombe hizo mbaya hadi ndani ya baa hatutakuwa na kero hii,” akasema Bw Wanyoike.