Michezo

Muungano wa wawaniaji kiti cha urais FKF wanukia

May 26th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MUUNGANO mpya miongoni mwa wawaniaji wa kiti cha urais Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) katika uchaguzi ujao wa kitaifa sasa unanukia.

Hii ni baada ya Katibu Mkuu wa zamani wa Cecafa Nicholas Musonye, Naibu Rais wa zamani wa FKF Sammy Shollei na mwaniaji wa zamani wa urais wa FKF Hussein Mohammed kufichua azma ya kuungana ili kumdengua Rais wa sasa, Nick Mwendwa anayepania kuutetea wadhifa wake katika uchaguzi huo.

Musonye na Shollei waliandaa kikao cha pamoja mnamo Jumatatu jioni jijini Nairobi katika hatua ambayo ililenga kujadili uwezekano wa Shollei na Mohammed kuzima maazimio yao ya kuendea urais wa FKF na badala yake kumwachia Musonye awanie wadhifa huo na washindani wengine.

Kwa mujibu wa mikakati na mpangilio mpya wa watatu hao, Mohammed anapigiwa upatu kukiendea kiti cha Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF naye Shollei awanie nafasi ya kuwa Naibu Rais.

Uchaguzi wa kitaifa wa FKF uliokuwa ufanyike mnamo Machi 2020, kwa sasa umefutiliwa mbali mara mbili huku vinara wa Shirikisho la Soka la Duniani (FIFA) wakipendekeza kuandaliwa kwa mkutano kati yao na Serikali ya Kenya na baadhi ya washikadau wa soka ili kufanikisha uchaguzi utakaotawaliwa na haki na usawa.

Mwendwa kwa sasa anachunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Kesi za Jinai (DCI) kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya Sh244 milioni zilizotolewa na serikali mwaka uliopita kwa minajili ya kuiandaa Harambee Stars kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri.

Mbali na kutowajibikia Sh125 milioni za basi ambalo lilinunuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa minajili ya kuchangia maendeleo ya soka ya Kenya, FKF pia haijalipa bonasi za wanasoka wa Stars na imeshindwa kuwalipa makocha wa zamani wa Stars Adel Amrouche, Bobby Williamson na Sebastien Migne kima cha Sh170 milioni.

Uamuzi wa Jopo la Mizozo ya Spoti (SDT) kuhusiana pia na uhalali wa kuendelea kuwepo kwa maafisa wa FKF ofisini licha ya awamu yao ya uongozi kutamatika rasmi mnamo Februari 10, 2020 unatazamiwa kutolewa wiki hii.

Mbali na Musonye, wawaniaji wengine wa urais wa FKF wanaolenga kubandua Mwendwa ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya St Peters Mumias Cosmas Nabongolo, aliyekuwa Mwenyekiti wa FKF Sam Nyamweya, Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Lordvick Aduda na aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa FKF, Twaha Mbarak.