Habari za Kitaifa

Muuza dhahabu feki aachiliwa kwa dhamana

April 14th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA anayeshtakiwa kupokea kitita cha Dola za Amerika (USD) 250, 000 (KSh37.5 milioni) ameachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa taslimu baada ya kuzuiliwa gerezani kwa siku mbili.

Nashon Otieno Agudha aliyeshtakiwa kwa kumdanganya muuzaji Johari wa Dubai Surrinder Singh Kanda aliachiliwa na hakimu mwandamizi Gilbert Shikwe mnamo Ijumaa, Aprili 12, 2024.

Agudha alikana kumtapeli Surinder pesa hizo akidai alikuwa na uwezo kumsafirishia kilo 300 za dhahabu kwa ndege ya kibinafsi kutoka Kenya hadi Dubai.

Agudha aliyekuwa amejikwatua suti na kufunga tai na saa ya bei ghali, alipelekwa gerezani baada ya Shikwe kusema alihitaji muda kutathmini ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana akidai sio buheri wa afya.

Kiongozi wa mashtaka Bi Judy Koech hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Agudha alikana kumlaghai Bw Surrinder Singh Kanda Dola za Amerika, USD 250, 000 sawa na Sh37, 500, 000, thamani ya Kenya, akidai alikuwa na uwezo kumsafirishia kutoka Kenya hadi Dubai kilo 300 za dhahabu.

Akipokea pesa hizo mshtakiwa alidai atakodisha ndege kwa minajili ya shughuli hiyo.

Pia mshtakiwa alimweleza mlalamishi Kanda kwamba atalipia dhahabu hiyo bima ili ikipotea afidiwe.

Mbali na matamshi hayo matamu kama asali, mshtakiwa alimweleza mlalamishi atalipia dhahabu hiyo kodi katika Mamlaka ya Ushuru nchini – KRA.

Hakimu alifahamishwa maneno hayo yote yalikuwa ni ubatili mtupu.

Muuzaji huyu wa dhahabu feki alikana kuwa alipokea pesa hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Surrinder Singh Kanda kati ya Julai 13 na Oktoba 18, 2023.

Mshtakiwa alisemekana alipokea pesa hizo katika mtaa wa kifahari wa Runda Glory Valley ulioko jijini Nairobi.

Akiwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana, Agudha alimweleza hakimu kwamba sio buheri wa afya na anahitaji tiba ya dharura katika hospitali ya kibinafsi.

“Madaktari katika hospitali za umma wamegoma na ninahitaji tiba ya dharura. Naomba uniachilie kwa dhamana nisiumie nikiwa gerezani,” Agudha alimsihi hakimu.

Mbali na ombi hilo, mshtakiwa alijulisha mahakama kwamba polisi walitwaa simu zake tatu za mkono, pamoja na gari lake la kifahari muundo wa Toyota V8.

Mshtakiwa alieleza hakimu kuwa simu na gari havina uhusiano na biashara hiyo ya dhahabu kati yake na Kanda.

Lakini kiongozi wa mashtaka Judy Koech aliomba mahakama imwachilie kwa kiwango cha juu cha dhamana, ikitiliwa maanani mshtakiwa alimghai muwekezaji huyo wa Dubai kiwango kikubwa cha pesa.

Bi Koech alisema mshtakiwa hajawasilisha mahakamani ushahidi kutoka hospitali kwamba anaugua.

Katika uamuzi wake, Bw Shikwe alisema “ninahitaji muda kutathmini mawasilisho ya pande zote. Nitatoa uamuzi Ijumaa. Mshtakiwa atazuiliwa gerezani.”

Punde tu baada ya hakimu kusema hayo mshtakiwa alimpelekea nduguye simu yake kisha akatiwa pingu na maafisa wa polisi na kupelekwa korokoroni.

Atarudishwa tena kortini Aprili 26, 2024 kutengewa siku ya kuskizwa