Habari Mseto

Muuza vipuri wa River Road kizimbani kwa kuiba mali ya wakili

April 15th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MUUZAJI wa vipuri vya simu eneo la River Road jijini Nairobi alishtakiwa Jumatatu kwa kuvunja afisi ya wakili na kuiba Sh20,000 na bidhaa nyingenezo zikiwamo jezi za michezo.

George Ochieng Owino alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Kennedy Cheruiyot na kusomewa mashtaka ya kuvunja afisi kuiba na kupatikana na mali iliyoibwa katika afisi ya wakili P K Kamau.

Bw Owino alikanusha mashtaka kuwa mnamo usiku wa Machi 11/12 katika jengo la Jubilee Insurance jijini Nairobi alivunja afisi ya Bw Kamau na kuiba mle ndani.

Alidaiwa aliiba Sh20,000, tarakilishi , jezi za michezo, viatu muundo wa Nike, kitabu cha hundi chenye kurasa 50. Jumla thamani ya bidhaa zilizoibwa ni Sh358,000.

Shtaka la pili dhidi yake lilisema kuwa mnamo Aprili 12, 2019 katika barabara ya Luthuli alikutwa na hundi mbili za Bw Kamau alizojua zimeibwa ama kupatikana kwa njia isiyo halali.

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh30,000 baada ya kumlilia aipunguze kutoka Sh100,000.