Habari Mseto

Muuzaji mafuta pabaya kwa kuiba mamilioni ya KCB

November 22nd, 2019 1 min read

Leonard Ndunda Kivuva akiwa kortini Alhamisi kwa kosa la kuibia benki ya Kenya Commercial Bank (KCB) zaidi ya Sh10m. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kampuni ya mafuta alishtakiwa Alhamisi kwa wizi wa zaidi ya Sh10 milioni kutoka benki ya Kenya Commercial.

Leonard Ndunda Kivuva alikanusha shtaka alilofunguliwa na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) la wizi wa Sh10,268,160 kutoka benki ya KCB tawi la Lavington, Kaunti ya Nairobi.

Kiongozi wa mashtaka Everlyne Maika alimweleza hakimu mwandamizi Bernard Ochou kuwa Kivuva anadaiwa aliiba pesa hizo kati ya Novemba 1 na 13, 2019.

Wakili Samson Nyaberi anayemwakilisha Bw Kivuva aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “ mushkil ulitokea wakati wa utekelezaji kazi na kwamba mshtakiwa hakuiba ila ni benki ilituma kimakosa pesa hizo.”

Bw Nyaberi aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana.

Hakimu alimwagiza mshtakiwa alipe dhamana ya Sh800,000 pesa tasilimu.

Kesi itasikizwa Januari 16, 2020.