Michezo

Muyoti pazuri zaidi kuwa mrithi wa kocha Fred Ambani aliyetimuliwa na Wazito FC

November 12th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Wazito FC kimeanza kuvizia wakufunzi Nicholas Muyoti na Jeff Odongo ili wajaze nafasi zilizoachwa wazi na Fred Ambani na Salim Babu.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kiufundi wa Wazito FC, Stephen Ochiel, kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL) kimepiga hatua kubwa katika kumshawishi Muyoti wa Kakamega Homeboyz awe mkufunzi mkuu akisaidiwa na Odongo aliyewahi kuwa kocha msaidizi kambini mwa Kisumu All Stars na Muhoroni Youth.

Hata hivyo, Muyoti amewataka Wazito FC kusitisha mwanzo mipango ya kumwajiri hadi mazishi ya baba yake mzazi yatakapokamilika.

“Ni ukweli kwamba vinara wa Wazito wamenipa ofa ya kujiunga nao. Hata hivyo, nimewaomba nikamilishe kwanza shughuli za maziko ndipo nitathmini hali ilivyo na kuona uwezekano wa kujadiliana nao,” akasema mwanasoka huyo wa zamani wa Thika United, AFC Leopards, Nzoia Sugar na Harambee Stars katika mahojiano yake na Taifa Leo.

Kwa upande wake, Cleophas Shimanyula ambaye ni mweyekiti wa Homeboyz amesema kwamba hatamzuia Muyoti kujiunga na Wazito FC ila akaonya kwamba hatashangazwa iwapo wakwasi hao watampiga kalamu baada ya kipindi kifupi jinsi Ambani alivyofanyiwa miezi mitatu tu baada ya kumrithi Stewart Hall aliyewahi pia kuwanoa AFC Leopards.

Wazito FC tayari wamemteua kipa wa zamani wa Harambee Stars, Matthew Ottamax, kuwa kocha mpya wa makipa kambini mwao.

Mlinda-lango huyo veterani amethibitisha uteuzi wake kupitia mtandao wa Facebook kwa kuandika: “Kiti moto cha ukufunzi kambini mwa Wazito sasa kinakutana na joto lenyewe. Tusubiri tuone nani mkali!”

Ottamax ambaye pia amewahi kunoa makipa wa AFC Leopards na Gor Mahia, anajaza pengo la Elias Otieno ambaye alitimuliwa kwa pamoja na Ambani na msaidizi wake Babu mnamo mnamo Novemba 9, 2020.

Watatu hao walifurushwa na Wazito FC siku chache baada ya kuongoza mabwanyenye hao wanaomilikiwa na mfanyabiashara Ricardo Badoer kusajili ushindi wa 2-1 na 5-1 dhidi ya Zoo Kericho FC na Narok Combined mtawalia kwenye mechi za kirafiki ugani Narok.

Ochiel ameshikilia kwamba kutimuliwa kwa Ambani na wenzake kulichangiwa na mizozo ya mara kwa mara kati ya benchi ya kiufundi na wachezaji, kisa cha hivi karibuni kikiwa kile kilichoshuhudia wanasoka 19 pekee kati ya 31 wakifika uwanjani kwa mechi za kirafiki dhidi ya Zoo.

Ingawa hivyo, Ambani ambaye ni kocha wa sita baada ya Stanley Okumbi, Fred Ouna, Hamisi Abdalla, Melis Medo na Stewart Hall kudhibiti mikoba ya Wazito chini ya kipindi cha misimu miwili, amelalamikia mazingira mabovu ya kufanyia kazi na maamuzi muhimu – yakiwemo ya kusajili wanasoka wapya – kufanywa bila ya makocha kuhusishwa.

“Pamekuwa na mizozo ya mara kwa mara katika ya usimamizi wa klabu na benchi ya kiufundi. Kikosi kimekuwa kikiendeshwa visivyo, na kilele cha hayo ni tukio la hivi majuzi lililoshuhudia usimamizi, chini ya mkurugenzi wa kiufundi, Ochiel, ukisajili idadi kubwa ya wachezaji bila ya kuhusisha makocha wanaoelewa mahitaji ya kikosi katika kila idara ugani,” akasema Ambani katika mahojiano yake na Taifa Leo.

“Mazingira ya kufanyia kazi kambini mwa Wazito FC ni mabovu na wakufunzi hawana usemi hata kidogo kuhusu hata mienendo na nidhamu ya wachezaji kambini. Ni kinaya kikubwa kwa usimamizi kutaka matokeo bora kutoka kwa benchi ya kiufundi wakati ambapo makocha wananyimwa uhuru wa kufanya maamuzi muhimu inayohusiana na kazi yao,” akaongeza mchezaji huyo wa zamani wa Harambee Stars.

Wazito FC watakuwa sasa wakitumia uga huo kwa mechi zao za nyumbani katika kampeni zijazo za FKFPL baada ya kusitisha shughuli katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Wazito FC, Dennis Gicheru, hatua yao hiyo ya kuhamia Narok Stadium ilichochewa na haja ya kupanua wigo wa mashabiki wao na kuchangia pia makuzi ya vipaji vya soka miongoni mwa chipukizi katika eneo zima la Narok.

Kwa upande wake, Babu alisema: “Yasikitisha kwamba imetulazimu kuagana na Wazito FC wakati ambapo tumeanza tu kukiandaa kikosi kwa minajili ya msimu mpya. Inakera kuona jinsi baadhi ya wachezaji walivyosajiliwa bila wakufunzi kuhusishwa moja kwa moja.”

Babu ambaye ni beki wa zamani wa Harambee Stars, alijiunga na Wazito FC mnamo Agosti baada ya kukatiza uhusiano na Western Stima alikokuwa kocha mkuu. Alianza ukufunzi wake katika kikosi cha mabingwa wa KPL 2006, SoNy Sugar akiwa kocha msaidizi pindi baada ya kustaafu soka. Alikwezwa baadaye kuwa mkufunzi mkuu wa kikosi hicho kabla ya kuyoyomea Migori Youth kisha Stima.

Katika kampeni za KPL msimu wa 2018-19, Babu alitawazwa Kocha Bora wa Mwezi mara mbili huku aliyekuwa mkufunzi wa Gor Mahia, Steven Polack akitwaa tuzo hiyo mara tatu.

Iwapo Muyoti na Odongo watatua Wazito FC, basi watasaidiwa kazi na wanasoka wa zamani wa kikosi hicho, Eric ‘Ero’ Odhiambo na David Oswe waliostaafu mnamo Septemba na kupokezwa majukumu kwenye benchi ya kiufundi.

Wazito FC, AFC Leopards, Western Stima na Gor Mahia na ni miongoni mwa klabu za FKFPL zilizojishughulisha zaidi sokoni katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji kwa minajili ya kampeni za msimu mpya wa 2020-21.

Wazito FC walisajili wanasoka 15 wapya kujaza mapengo ya wachezaji 14 waliobanduka kambini mwao.

Wanasoka hao ni pamoja na Kevin Kimani (Mathare United FC), Mark Hezbon, Ronald Otieno (Kisumu Allstars FC), Vincent Oburu (AFC Leopards), Boniface Omondi (Gor Mahia), Castro Ogendo (Bidco United), Edwin Odhiambo (Western Stima), Fidel Origa (Western Stima), Fredrick Odhiambo (Gor Mahia) na Kevin Okumu (Nairobi City Stars).

Wengine ni Maurice Ojwang (Western Stima), Michael Owino (Kisumu Allstars), Stephen Otieno (Western Stima), Clinton Okoth (Migori Youth) na Jackson Juma (Soy United).