Bambika

Muziki mtamu unahitaji msanii aliyeenda shule – Span One

March 13th, 2024 2 min read

NA BENSON MATHEKA

MWANAMUZIKI Lamaz Mbago Omollo almaarufu Span One amesema lengo lake katika tasnia ya muziki ni kuondoa fikra na dhana kwamba burudani ni uhuni.

Ni miaka saba sasa tangu msanii Span One ajitose rasmi katika bahari ya muziki. Yeye ni mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Na licha ya kufumua vibao vingi na jina lake kutamba kwingi, anasema hajachoka kupiga mbizi kamwe.

“Ningali imara kuogelea katika bahari hii pana ya muziki.

Nina nguvu za kutosha na sauti ya kuburudisha. Ninaupenda muziki na sitauacha,” asema msanii huyu anayetambuliwa kwa makeke yake akiwa jukwaani.

Msanii Span One asema kuwa kabla ya kujiunga na ulimwengu wa muziki, alikuwa mwigizaji maarufu, kipawa ambacho kiliota mizizi akiwa shuleni.

“Niliishindia shule yangu tuzo nyingi kwa sababu ya uigizaji,” asema.

Ni mwaka 2003 ambapo alikutana na rafiki yake mmoja kwa jina NV aliyemshawishi ajiunge na muziki. Tayari msanii NV alikuwa amebobea katika fani hii na bila kusita, Span One alikata kauli kujiunga na muziki.

Kwa pamoja, waliunda kikundi kilichojulikana kama Holy Bullets kilichoandaa vibao vya Injili kwa kutumia midundo ya kizazi kipya.

Span One asema kikundi hicho kilichomshirikisha msanii Sinkiller, kilitia fora kwa kufumua vibao vilivyoangazia maisha ya kiroho kwa vijana.

“Tulillenga kuwahimiza vijana wasipuuze Neno la Mungu. Tulifanya hivyo kupitia mitindo ya muziki wanayoipenda na tulifaulu,” asema.

Baadhi ya vibao walivyofumua ni kile kibao maarufu kwa jina ‘You Are Mine’. Kibao hicho kilitawala chati za vibao bora vya Injili mwaka 2005.

Kikundi hicho kilipotawanyika mwishoni mwa 2006, Span One aliendelea kuwasha moto wa burudani kwa kuimba nyimbo na kuandaa shoo zilizovutia mashabiki tele.

“Nilikuwa nimeamua sitarudi nyuma hivyo kujitolea kwa moyo wangu wote kushiriki muziki,” asema.

Mnamo 2008, alialikwa kushiriki jukwaa moja na mwanamuziki wa kitamataifa Kirk Franklin katika tamasha za ‘Extreme Weekend’ jijini Nairobi.

Anasema mwaliko huo, ulibadilisha maisha yake katika muziki.  Mialiko ya kuenda kuburudisha ilianza kumiminika kwake.

“Nilipowasha moto wa burudani, mashabiki walinishangilia na ukawa mwanzo mpya katika maisha yangu ya usanii. Nilianza kupokea mialiko ya kwenda kutumbuiza mbali na karibu,” asema Spanone ambaye kibao chake kwa jina ‘Yuko Juu’ ni miongoni kwa vile vinavyotawala chati katika vyombo vya habari kwa wakati huu.

Mbali na kutumbuiza na kufumua vibao, Span One ana mipango ya kupalilia vipawa vya wanamuziki chipukizi nchini. Amekuwa akitembelea vyuo vikuu, shule za upili na makanisa kuwahamasisha vijana umuhimu wa muziki katika maisha yao.

“Lengo langu ni kuwatayarisha vijana walio na vipawa ili wavitumie ipasavyo. Wengi waliojaliwa vipaji hukosa mwongozo wakitoka shule na vipawa hivyo huangamia,” asema.

“Nataka kubadilisha dhana ya wengi kwamba muziki ni uhuni. Ninawahamasisha vijana walio katika taasisi za elimu jinsi ambavyo wanaweza kutumia fani hii kuwajengea msingi imara maishani,” aongeza.

Mwanamuziki huyo asema njia ya pekee ya kujenga jamii yenye kuwajibika ni kuwatayarisha vijana kukuza vipawa vyao.

“Vijana wengi  walio na vipawa vya muziki huvunjwa moyo na  wazazi au jamaa wa karibu kwa kuwaambia hauwezi kuwapa ajira. Huu ni upuzi. Muziki ni taaluma kama zile nyingine,” asema.

Hata hivyo, anawashauri vijana watie bidii masomoni hata kama wanahisi kuwa wamejaliwa vipawa akisema kuwa nyakati ambazo vijana walitoroka masomo kucheza muziki umepita.

“Siku hizi muziki unaandaliwa kupitia tekinilojia ya kisasa inayohitaji mtu aliyebobea kielimu,” asema msanii ambaye vibao vyake, ‘The Truth’ na ‘Cross Movement’ vinapendwa mno.