Makala

'Muziki una raha na karaha zake'

August 8th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MSANII Patrick Mwangi anakiri kuwa sekta ya muziki nchini ina raha na karaha zake.

Anasema tajriba yake ya miaka 11 katika sekta hii inafanya asimulie yale amekumbana nayo; hali ambazo zinaweza zikawa shimo refu na pana kwa vijana, lakini pia kupata pesa za kiasi cha kufurahisha.

“Acha nikusimulie. Katika sekta hii ya muziki, mapenzi haramu na ya kiholela yako kwa wingi. Fahamu kuwa hii ni sekta ya anasa ambapo ulevi, utumiaji mihadarati na kujiachilia ni nguzo,” anasema Mwangi.

Anasema wanamuziki ambao hupata umaarufu yaani ‘celebs’ hujipata wakiwindwa kila kona na walio na nia ya kuwageuza mlo kitandani.

“Wanaume kwa wanawake huwa katika hatari hii. Kijana mwanamume akiwika zaidi, mapenzi ndiyo hayo yanamwandama kutoka kwa mashabiki wa kike huku naye wa kike akiwika, anajipata akichumbiwa kutoka kila kona na wanaume,” anasema.

Anasema pia visa vya ushoga na usagaji vimejaa katika sekta hii na ni juu ya mwanamuziki binafsi kuchukua tahadhari na kujiweka salama katika safu hii.

Bw Mwangi ambaye jina lake la usanii ni Muraya Junior anasema kitu kingine ambacho huangamiza wengi wa vijana katika sekta hii ni mikopo ili waafikie maisha ya umaarufu.

Asema: “Kijana akishatoa wimbo anaanza kukimbizana na mikopo ili ajipe gari, mikufu almaarufu bling bling, mavazi, uwezo wa kuburudisha marafiki na pia kujiangazia kama aliyefanikiwa kimaisha. Hatimaye ngoma inakosa kuunda pesa hizo na unampata kijana anaanza kufilisika.”

Anasema kuwa yule kijana ambaye atabakia akiwa wima katika sekta hii ni yule tu ambaye atabakia katika mkondo wa usawa na haki katika hali zote za safu hii.

“Wale ambao wataingia katika safu hii wakisaka anasa wataangamia. Wale ambao wataingia katika safu hii wakisaka riziki halali wataingia katika madaftari ya Wakenya waliobarikiwa na talanta ya kimuziki ambao walijisaidia, lakini wengine watahesabiwa kama takwimu katika makaburi ya Kenya,” anasema.

Anakiri kuwa katika sekta ya muziki nchini na kwingineko kumejaaa visa vya ushirikina kiasi kwamba “wengi wamefilisika wakigharimia kugangwa ili wawike kimuziki na pia wakiganga kazi zao ziwe na ufuasi sokoni.”

Anasema kuwa hali hii ya ushirikina katika muziki imehusishwa na mauti ya wengi wa wanamuziki chipukizi ambao wakionyesha dalili za kufanikiwa wanarushiwa ndumba na wanaangamia ghafla.

Pia anateta kuwa wizi wa kazi za sanaa ni changamoto kubwa ambayo inafaa kushughulikiwa kwa kuwa inafukarisha wengi chipukizi.

“Utatoa ngoma yako leo asubuhi na kabla uuze kanda moja, wezi wa kurekodi wameuza kanda 1,000 katika maeneo mengi ya nchi. Ukienda sokoni kujitambulisha ukiwa na matumaini ya kuuza kanda kadhaa, unapata tayari wateja washainunua kutoka kwa wezi hao,” anasema.

Hata hivyo, anashabikia upenyo wa soko jipya la kimitandao ambapo majukwaa kama YouTube na Skiza yanaendelea kuwafaa wanamuziki kwa pato la uhakika.

Mawaidha yake ya dhati ni kuwa wasanii wazingatie utu na “tuenzi Mungu kama mleta baraka yetu.”