Mvita yawaniwa vikali Nassir akijiondoa

Mvita yawaniwa vikali Nassir akijiondoa

Na FARHIYA HUSSEIN

SIASA za ubabe zimepamba moto katika eneobunge la Mvita, Kaunti ya Mombasa, wakati ambapo mbunge wa sasa, Bw Abdulswamad Nassir amepanga kuwania ugavana mwaka 2022 na hivyo kuacha nafasi ya ubunge wazi.

Kufikia sasa, wanasiasa kadhaa wakiwemo Omar Shallo, Mohammed Machele, Hassan Sumba na Said Twaha wametangaza azimio lao kushindania kiti hicho cha ubunge.

Bw Shallo ambaye ni mfanyabiashara, atakuwa anajaribu bahati yake katika kinyang’anyiro hicho kwa mara ya pili bada ya kuibuka wa pili katika uchaguzi wa 2017 ambapo aliwania kupitia Chama cha Jubilee.

Wakati huo, alifanikiwa kupata kura 11,063 dhidi ya Bw Nassir ambaye alishinda kwa kura 46,575 kwa mujibu wa takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mwanasiasa huyo anatarajiwa kutumia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuwania ubunge Mvita mwaka 2022.

“Naamini Bw Nassir ameleta mafanikio bora katika elimu. Lakini sekta ya kibiashara bado haijatiliwa maanani ipasavyo na hapo ndipo nalenga kuboresha. Kuna biashara nyingi ndogondogo katika eneobunge la Mvita ambazo zinahitaji kuwezeshwa kustawi,” akasema.

Alisema uamuzi wake kujiunga na UDA ni kwa vile hajaona kama ODM ina maono bora ya kuleta mabadiliko ambayo yatawafaa wananchi.

Kwa upande wake, Bw Machele ambaye ni mara yake ya kwanza kuwania kiti cha kisiasa alisema yuko tayari kwa ushindani atakaopata katika azimio lake.

Ijapokuwa amekuwa akionekana kuwa karibu na baadhi ya wandani wa mwaniaji tikiti ya ODM kwa ugavana Suleiman Shahbal, mwanasiasa huyo ambaye hufahamika kwa shughuli anazoendeleza kupitia kwa Wakfu wa Machele alisisitiza anajitegemea.

“Niko katika kinyang’anyiro cha ubunge Mvita 2022 na sitegemei mtu yeyote,” alisema alipohudhuria mkutano katika ukumbi wa Majengo.

Mwandani wa Bw Shahbal ambaye aliomba kutotajwa jina gazetini na mtandaoni kwa vile hana idhini ya kuzungumzia mipango yake ya kisiasa, alisema kwa sasa hampendelei mwaniaji yeyote kwa vile chama chake cha ODM hakijatangaza atakayewania kiti hicho.

“Shahbal ataunga mkono mwaniaji ubunge atakayepeperusha bendera ya ODM na kwa sasa, hakuna yeyote,” akasema.

Bw Nassir pia hajatangaza mwanasiasa yeyote ambaye angependa arithi kiti hicho, anapojipigia debe kurithi kiti kitakachoachwa wazi na Gavana Hassan Joho.

Wakati huo huo, Waziri wa Uchukuzi, Miundomsingi na Ujenzi katika Kaunti ya Mombasa, Bw Taufiq Balala, alikana madai kuwa amepanga kutafuta tikiti ya ODM ili kuwania ubunge Mvita.

You can share this post!

NGILA: Kupotea kwa huduma za Facebook kuwe funzo

Utekaji nyara uliozidi Mlimani wazua hofu