Habari za Kitaifa

Mvua: Biashara zatatizika kati ya Kenya, Sudan Kusini

May 7th, 2024 3 min read

NA OSCAR KAKAI

TANGU barabara kuu ya Kitale-Lodwar–Juba kukatika eneo la Lous, katika kaunti ya Pokot Magharibi, uchumi umeathirika eneo hilo kuingia nchi jirani, biashara zikiharibika kutokana na mvua kubwa inayonyesha.

Barabara hiyo ndio njia rahisi inayounganisha Kenya na Sudan Kusini na hali yake kwa sasa imeathiri biashara kati ya nchi hizi mbili.

Aidha, hali hii imewazuia wafanyabiashara kutoka Kaunti ya Turkana na nchi ya Sudan kuendelea na kazi yao ya kawaida.

Hali hiyo imelazimu matrela makubwa na magari madogo kungoja kwa siku kadhaa, barabara ikikarabatiwa.

Kwa sasa, wafanyabiashara wanaohudumu kwenye barabara hiyo wanaitaka serikali kuharakisha ukarabati ili shughuli za kawaida kurejea.

Uchunguzi unaonyesha kuwa wafanyabiashara wa kutoka Kenya wanapata ugumu kufika nchini Sudan Kusini.

Bw Simon Tumkou, ambaye ni mfanyabiashara kutoka mji wa Kapenguria, anasema kuwa wenzake wengi wameamua kutumia njia ya Uganda kupitia Mbale, Lira-Gulu na Kabong hadi nchini Sudan Kusini.

“Ni vigumu sasa kutumia njia ya Logichogio wakati huu wa masika. Unaweza kuishi njiani kwa wiki mbili,” anasema Bw Tumkou.

Wafanyabiashara wengi husafirisha nafaka kama mahindi na mboga na matunda, lakini pia bidhaa za ujenzi hadi nchini Sudan Kusini.

Wafanyabiashara ambao wanauza vyakula kama nyanya na mboga kutoka miji ya Kitale na Kapenguria kuelekea Lodwar, wanakadiria hasara kubwa kutokana na bidhaa hizo kuharibika ama kuoza kabla zifike penye zinapelekwa.

Hali hiyo imechangia uhaba wa chakula kushuhudiwa Turkana na eneo la Turkwel.

Wanasafiri kwenye barabara hiyo wanasema kuwa muda wa kawaida kutoka mji wa Kitale hadi Lokichogio ni siku mbili lakini sasa wanaishi njiani siku nne.

Bw John Chege, mfanyabiashara ambaye huenda Sudan Kusini, anasema imekuwa vigumu kwa matrela ya kubeba bidhaa kufanya kazi sababu ni vigumu kupita eneo la Lous na Lochwa.

“Bidhaa zangu zote na vyakula vilioza baada ya mimi kulala eneo la Kambi Karai wikendi,” akasema Bw Chege.

Naye Bi Alice Nanyama ambaye husambaza mboga kwenye miji ya Lodwar, Kakuma na Lokichogio, anasema kuwa amepata hasara kubwa.

“Pia tuko kwa hatari ya kuvamiwa na wahalifu kwenye barabara ambao hutupora,” akasema Bi Nanyama.

Bw John Ekai anasema kuwa hali hiyo imekuwa pigo.

“Ni shida kubwa sababu ya kuchelewa kwa wasafiri na bidhaa,” akasema Bw Ekai.

Mwenyekiti wa muunganao wa wafanyabiashara katika kaunti ya Pokot Magharibi (KCCI) Mark Lotee, anasema kuwa barabara hiyo imewavunja moyo wanachama ambao hutegemea kupata soko kutoka Sudan Kusini.

“Kaunti ya Turkana inategemea kupata vyakula kutoka Kitale, Kapenguria, Chepareria na Ortum,” anasema.

Anasema kuwa matrela mengi na matatu zimeondoka kwenye barabara hiyo.

“Wawekezaji wengi wameondoka na wale wanataka kuekeza Sudan Kusini wameshindwa kutokana na barabara hiyo mbovu,” anasema Bw Lotee.

Anasema kuwa serikali inafaa kukarabati barabara hiyo ili wakenya waweze kuekeza kwenye nchi hiyo jirani.

“Barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa nchi ambayo inakua ya Sudan Kusini ambapo Wakenya wanafaa kuwekeza,” anasema.

Magari mengi yameonekeana kwenye msongamano kwenye barabara hiyo.

Kafiu ambayo iko katika kaunti Ndogo ya Turkana Kusini baina ya Lokichar na Kainuk imechangia kuchelewa kwa usafiri na ongezeko la nauli na bei ghali ya kusafirisha bidhaa.

Matrela ambayo yamebeba bidhaa yameegeshwa kwenye miji ya Makutano, Ortum, na Kainuk.

Bw Dennis Omoi, dereva ambaye amekuwa akitumia barabara hiyo kwa miaka 20, ameelezea kughadhabishwa kwake na hali ya barabara hiyo kwa sasa.

‘‘Nimekuwa nikitafuta riziki kwenye barabara hii lakini wakati huu, mambo yamebadilika. Nimekuwa hapa kwa siku moja na nusu na bado tutalala tena eneo la Lochwaa kwa siku nyingine,’’ akasema Bw Omoi huku akiongeza anavumilia kijibaridi.

Hata hivyo, Halmashauri ya Ujenzi wa Barabara Kuu (KeNHA) imeanza kuunda barabara mbadala eneo la Lous na Kambi Karai katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Wahandisi wa KeNHA wako kwenye eneo hilo wakianza kukarabati barabara hiyo.

Tingatinga la KeNHA wakati wa ukarabati wa barabara. PICHA | OSCAR KAKAI

Mratibu wa KeNHA eneo la Kaskazini mwa Bonde la ufa Mhandisi Philemon Kipkoech anasema kuwa maafisa wa KeNHA wametumwa kwenye barabara hiyo kudhibiti msongamano wa magari kuzuia ajali.

Anasema kuwa njia hizo mbadala zitasaidia magari kupita vyema.

“Eneo moja la barabara mbadala linapitisha matrela na jingine ni la magari madogo,” akasema Bw Kipkoech.

Mhandisi huyo amewataka madereva wanaotumia barabara hiyo kuwa waangalifu kati ya eneo la Lous na Kambi Karai.

Jumamosi wasafiri wengi walikwama kwenye eneo hilo.

[email protected]