Habari Mseto

Mvua ilivyomsomba daktari na kuchochea stima kuua mwanamke Kakamega

May 6th, 2024 2 min read

NA SHABAN MAKOKHA

DAKTARI amefariki baada ya kusombwa na maji ya mto Lwang’ombe katika kijiji cha Ilala, kaunti ndogo ya Shinyalu huko Kakamega taifa linaposhuhudia kipindi cha janga la mafuriko.

Mwili wake ulipatikana siku moja baadaye ukiwa umenaswa katikati ya matawi ya mti uliomezwa na maji hayo.

Bw Ronald Salimu Musume, 72, daktari wa magonjwa ya akili, anaripotiwa kufa maji alipokuwa akijaribu kuvuka mkondo wa maji huku akikanyaga nguzo mbili zilizounganishwa na kingo za maji.

Kwa kawaida, wakazi ambao hawataki kutumia magari, hupendelea kutumia njia hii ya kuvuka mto.

Huwa njia ya mkato ya kufika Shirere watumiaji wanapoelekea mji wa  Kakamega.

Mkewe Dkt Musume, Fridah Okuku alisema marehemu aliondoka nyumbani kwao  Ijumaa asubuhi akielekea Kakamega.

Mkewe anasema alienda mjini kushughulikia ujenzi wa kituo cha kiafya cha kibinafsi ila hakurejea.

“Kwa kuwa tuna nyumba nyingine Kakamega, nilidhani alikuwa amelala mjini kwa sababu ya mvua kubwa iliyonyesha wiki nzima. Siku iliyofuata, nilimpigia simu lakini haikuingia. Nilisubiri nikijua yuko salama,” akasimulia Bi Okuku.

Mnamo Jumamosi, Bi Okuku alipokea simu kutoka kwa jirani yao akimjulisha kwamba mwili wa mumewe ulikuwa umepatikana majini, umbali wa mita 50 kutoka nyumbani kwao.

“Nilikuwa nimetoka shambani nilipopokea simu. Niliishiwa na nguvu na kukaa chini hata bila kuongea na aliyenipigia simu. Aliniita tena, akinielekeza nikimbilie mahali ambapo mwili wake ulikuwa. Niliweza kuamka na kujikongoja hadi eneo hilo,” alieleza.

Inakisiwa kuwa marehemu aliteleza na kuanguka kwenye maji yaliyokuwa yakienda kasi na kumsomba mvua kubwa ilivyonyesha. Wenyeji walisaidia kupata mwili huo.

Dkt Musume alikuwa daktari wa magonjwa ya akili katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega hadi 2021.

Kisha alistaafu na kufanya kazi katika zahanati ya kibinafsi mjini Kakamega.

Mwanawe mkubwa Albert Mandela alisema baba yao  alikuwa tegemeo la familia na kifo chake ni pigo kwa familia.

“Tumekuwa tukimtegemea kwa mahitaji ya familia. Hatujui tutaishi vipi sasa baada ya baba kufariki,” Bw Mandela alisikitika.

Katika kisa kingine, mwanamke mmoja alifariki baada ya kupigwa na umeme akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Matawa, mjini Mumias alipokuwa akifua nguo.

Bi Caroline Juma, 24, aliathiriwa na umeme alipogusa waya uliotumiwa kuwa laini ya kuanika nguo ambayo iliunganishwa na nyumba yake.

Baba mkwe wake, Odinga Juma, alisema binti huyo alikuwa akianika nguo akiwa hajavaa viatu kwenye mvua.

“Hatukujua kuwa mabati ya nyumba yake yalikuwa yakigusa waya wa umeme,” akasema Bw Odinga.

Jirani alimsikia akilia kwa uchungu na akakimbia kumsaidia lakini alikuwa ameganda alipofika. Kufikia wakati wa kuokolewa, hakuweza kusonga.

Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Mumias Magharibi Stephen Muoni amesema uchunguzi umeanza kubaini kama kumekuwa na muunganisho haramu wa umeme.

“Tunashuku kulikuwa na umeme uliounganishwa kwenye nyumba yake na mtu ambaye hajaidhinishwa kushughulikia stima. Inasikitisha sana kwamba alifariki lakini tumeanza uchunguzi,” akasema Bw Muoni.

Marehemu alipelekwa hadi Hospitali ya Jamia  mjini Mumias lakini alitangazwa kuwa amefariki alipofika.

TAFSIRI : LABAAN SHABAAN