Habari

Mvua iliyopitiliza kiwango imesababisha vifo vya zaidi ya watu 10, yasema idara husika

October 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MVUA iliyopitiliza kiwango inayoendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali nchini imesabisha vifo vya zaidi ya watu 10 huku wengine zaidi ya 1,000 wakiachwa bila makao.

Mali ya thamani kubwa pia imeharibiwa na mvua hii ambayo ilianza kunyesha kwa wingi majuma mawili yaliyopita.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa inasema mvua hiyo itaendelea kunyesha katika sehemu kadha nchini katika kipindi cha siku tano zijazo.

Mvua kubwa itashuhudiwa katika sehemu za Kaskazini Mashariki, nyanda za juu Mashariki na Magharibi mwa Rift Valley, Kaskazini Magharibi mwa nchini, Pwani na maeneo ya Kusini Mashariki mwa nchini.

“Kaunti ambazo zitashuhudia mvua iliyopitiliza kiwango hadi Jumatano ni pamoja na Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, Isiolo, Nairobi, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka Nithi, Turkana, West Pokot na Samburu,” akasema mkurugenzi wa idara hiyo Stella Aura kwenye taarifa aliyotoa Jumatatu.

Maeneo mengine ambayo yataendelea kushuhudia mvua kubwa, kulingana na afisa huyo, ni Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, Taita Tavata pamoja na maeneo ya ukanda wa pwani kama vile kaunti za Tana River, Kilifi, Lamu, Kwale na Lamu.

Bi Aura anasema upepo mkali utarajiwa kuvuma kwa kasi ya mita 12,5 kwa sekunde katika maeneo ya Kaskazini Magharini na Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Mkurugenzi huyo ameonya wakazi wanaoishi katika maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi kuhamia katika maeneo ya salama ili kujiupusha na hatari.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa yatoa takwimu za maafa

Mvua iliyopitiliza kiwango imesababisha maafa mengi kwa mujibu wa idara ya utabiri wa hali ya hewa.

Watu wanne wa familia moja waliuawa na maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Turung, Marakwet Mashariki, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, mnamo Alhamisi, Oktoba 17, 2019.

Watu wanne walifariki katika Kaunti ya Meru mnamo Oktoba 17 baada ya kusombwa na maji ya mafuriko.

Mtu mmoja alithibitishwa kufariki na wengine watano hawajulikiani waliko katika Kauti ya Kitui baada ya gari walimokuwa wakisafiria kusombwa na mafuriko mnamo Oktoba 16, kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Mtu mmoja amefariki katika Kaunti ya Wajir baada ya kusombwa na maji ya mafuriko. Mifugo 900 pia inahofiwa iliangamia.