Habari

Mvua iliyopitiliza kiwango yasababisha hasara tele

October 21st, 2019 2 min read

Na WANDISHI WETU

MVUA ilizidi kusababisha uharibifu na hasara usiku wa kuamkia Jumapili, huku onyo likitolewa kwamba baadhi ya maeneo yataendelea kupokea mvua iliyopitiliza kiwango kwa muda wa mwezi mzima.

Hata hivyo, maeneo mengine kama vile Nairobi na Mombasa yalipata afueni kwani mvua ilipungua baada ya kunyesha kwa wingi tangu Alhamisi wiki iliyopita.

Katika Kaunti ya Isiolo, wafugaji wameonywa dhidi ya kuchunga mifugo yao karibu na Mto Ewaso Nyiro ili kuepuka uwezekano wa kusombwa na mafuriko.

Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa wa Isiolo John Nguyo aliwataka wakazi wanaoishi karibu na mto huo, ambao ni wa pili kwa urefu nchini, kuhamia katika maeneo salama.

“Mvua kubwa itasababisha mafuriko katika maeneo yaliyo karibu na mito ya Ewaso Nyiro na Isiolo na tunawashauri wachungaji wa mifugo na wakazi kuhamia maeneo mengineyo kuepuka kupoteza maisha na mali yao,” akasema Bw Nguyo.

Maeneo yanayotarajiwa kuathiriwa na mafuriko ni Malkadaka, Galfarsa, Kinna, Sericho, Oldonyiro na Garbatulla.

Akihutubia wanahabari mjini Isiolo, Bw Nguyo aliwataka wakulima kutoka maeneo ya Cherab na Chari kupanda haraka ili wanufaike na mvua inayoendelea kunyesha.

Wakazi wa mjini Isiolo pia wametakiwa kuwa na tahadhari kutokana na uwezekano wa kutokea kwa mafuriko ambayo huenda yakasababishwa na maji yanayotiririka kutoka kaunti jirani ya Meru.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa pia iliitaka wizara ya Afya ya Kaunti ya Isiolo kujiandaa ili kuweza kukabiliana na mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu.

Kwingineko, wakazi wa eneo la Muthwani wilayani Mavoko wameitaka serikali ya Kaunti ya Machakos kukarabati barabara ambazo zimeharibiwa na mvua kubwa ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika eneo hilo. Wito huo ulitolewa huku baadhi ya wakuu wa shule wakihofia kuwa huenda mvua inayonyesha ikatatiza kufanyika kwa mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) katika baadhi ya maeneo.

Katika Kaunti ya Pokot Magharibi, watoto wawili walifariki huku watu wengine wa familia yao kujeruhiwa kufuatia mkasa wa maporomoko ya ardhi kijijini Solion, eneobunge la Sigor, Ijumaa usiku.

Watoto hao wawili wenye umri wa miaka miwili na mitatu walizikwa kwenye tope wakiwa ndani ya nyumba huku wazazi wao wakiponea chupuchupu.

Mwili wafukuliwa

Mwili wa mvulana mwenye umri wa miaka mitatu ulifukuliwa kutoka kwenye tope huku mwili wa msichana mwenye umri wa miaka miwili bado upo kwenye tope huku maafisa wa polisi wakiendelea na juhudi za kuutafuta.

Akithibitisha mkasa huo, Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Pokot ya Kati Bw Were Simiyu alisema mkasa huo ulisababishwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha katika eneo hilo.

Alisema majeruhi wanaendelea kutibiwa katika hospitali ya Kapenguria.

“Miwili wa mvulana umehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Kapenguria. Maafisa wa usalama wanaendelea na shughuli ya kusaka maiti ya msichana,” akasema.

Waliojeruhiwa ni mama yao Lorna Limareng na watoto wengine wa umri wa miaka minne na minane.

Ripoti za Waweru Wairimu, Gastone Valusi na Oscar kakai