Habari Mseto

Mvua itanyesha kote nchini, Idara sasa yasema

April 23rd, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wananchi kote nchini wanatarajia kupata mvua juma hili, kila siku kwa siku tano zijazo, kulingana na taarifa ya hivi punde kuhusiana na hali ya hewa.

Pia, wanafaa kutarajia joto jingi, au baridi kupita kiasi katika kipindi hicho.

Katika taarifa ya Idara ya Kutabiri Hali ya Hewa (KMD), wiki hii itakuwa ni mvua nyingi, mvua ya rasharasha na joto lenye kubadilikabadilika kati ya nyuzi tano katika eneo la Kati na Nairobi na nyuzi 40 katika maeneo ya kaskazini.

Utabiri huo wa wiki moja, hadi Jumamosi Aprili 27, unaonyesha kuwa katika maeneo mengi, mvua itakuwa ikishuhudiwa nyakati za asubuhi katika “maeneo kadhaa” na rasharasha zitashuhudiwa wakati wa adhuhuri.

Lakini mvua itapungua kuanzia Jumanne wiki ijayo, alisema Bw Bernard Chanzu, kaimu naibu mkurugenzi wa KMD.

Mvua haitanyesha kila siku kuanzia siku hiyo, lakini kutakuwa na nyakati kavu na upungufu wa kiwango cha mvua, alisema.

“Takriban kufikia Jumatatu, tunatarajia mvua ya kadri au nyingi katika maeneo ya Magharibi, Nyanza, mpakani Moyale, Marsabit, Isiolo, Meru, Embu na eneo la nyanda za Kati,” alisema wakati wa mahojiano na Taifa Leo.

Wakazi wanaoishi karibu na Ziwa Victoria, nyanda za Magharibi mwa Bonde la Ufa na Bonde la Ufa kati na Kusini pia wanafaa kutarajia ngurumo za radi katika maeneo kadhaa wakati huo.

Mvua kubwa ya zaidi ya milimita 30 ilitarajiwa Magharibi mwa Kenya, eneo karibu na Ziwa Victoria, nyanda za Kati na baadhi ya maeneo ya Nairobi, kusini na kati Bonde la Ufa Jumatatu na Jumanne wiki hii.