Habari Mseto

Mvua kiwango kilichopitiliza kunyesha nchini, idara ya utabiri wa hali ya hewa yasema

November 25th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

MVUA ya kiwango kilichopitiliza inatarajiwa kunyesha sehemu nyingi nchini, idara ya utabiri wa hali ya hewa imesema.

Katika notisi, idara hiyo imesema mvua hiyo inatarajiwa kunyesha kuanzia Novemba 26 hadi Novemba 29 kwa kaunti zaidi ya 35.

Kulingana na watabiri wa hewa, mvua hiyo inatarajiwa kuanza kunyesha mnamo Novemba 26 katika maeneo yaliyoko eneo la Kaskazini Mashariki nchini, kisha itaongezeka na kuelekea upande wa Kusini Mashariki, Pwani, Magharibi na kati nchini ikiwemo maeneo ya Nairobi mnamo Novemba 27 na 28.

“Mvua hiyo ya Novemba inatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo ya Magharibi, Kusini Mashariki, Pwani na Kati ya nchi. Hata hivyo, itapungua mnamo Novemba 30,” imesema idara hiyo katika notisi.

Mvua hiyo inatarajiwa kunyesha katika kaunti za Mandera, Marsabit, Isiolo, Wajir, Garissa, Nyeri, Kiambu, Nyandarua, Laikipia, Murang’a, Embu, Meru, Kirinyaga, Tharaka-Nithi, na Nairobi.

Pia, kaunti za Taita-Taveta, Kajiado, Narok, Kitui, Machakos, Makueni, Kisii, Nyamira, Kericho, Bomet, Nakuru, Baringo, Migori, Nandi, Trans-Nzoia, Samburu, Elgeyo Marakwet na Uasin-Gishu.

Zaidi, mvua hiyo inatarajiwa katika kaunti za Vihiga, Bungoma, Homa Bay, Busia, Kisumu, Siaya, Kakamega, Mombasa, Kwale, Kilifi, Tana River na Lamu.

Wakazi wa maeneo hayo walionywa kuwa makini manake kuna uwezekano wa kuweko kwa mafuriko.

Pia, walionywa waepuke kuendesha magari au kutembea ndani ya maji barabarani, katika viwanja au kusimama chini ya miti wakati wa mvua ili kuepuka athari za mweso na ngurumo za radi.

“Zaidi, wavuvi wanafaa kuwa makini zaidi wanapofanya shughuli zao manake mawimbi yanatarajiwa katika bahari na maziwa. Zaidi, watu katika maeneo ambayo maporomoko ya ardhi hufanyika wanafaa kuchukua tahadhari mapema,” ikasema idara hiyo.