Habari Mseto

Mvua kubwa itaendelea kunyesha nchini – Idara

September 10th, 2019 1 min read

Na Siago Cece

MVUA kubwa inaendelea kushuhudiwa katika maeneo tofauti nchini ikiwemo sehemu za Nairobi, Kisumu, Bonde la Ufa, Magharibi na Pwani huku shughuli nyingi zikiathiriwa.

Katika eneo la Pwani, mvua hiyo imeathiri shughuli za kibiashara, huku magari ya uchukuzi yakiongeza naulu, na msongamano mkubwa kushuhudiwa katika barabara za jiji.

Idara ya hali ya anga nchini ilitabiri kuwa mvua itanyesha wiki moja hasa majira ya asubuhi katika sehemu nyingi nchini.

Maeneo ya Nyali, Kisauni, Mvita, Likoni, Changamwe na Jomvu katika Kaunti ya Mombasa yanatarajiwa kupokea mvua tele hasa wakati wa asubuhi kwa siku chache zijazo. Kaunti za Lamu, Kilifi na Kwale pia zimeshuhudia mvua kubwa.

“Kiwango cha mvua kitaongezeka kwa siku zijazo na mvua itanyesha asubuhi, mchana na usiku,” alisema msimamizi wa idara ya utabiri wa hali ya anga Mombasa, Bw Edward Ngure.

Wakati huo huo, wavuvi pamoja na waogeleaji wametahadharishwa kuhusu mawimbi na upepo mkali ufuoni.