Habari Mseto

Mvua kubwa Lamu yaharibu barabara

November 10th, 2020 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

MVUA kubwa ambayo imekuwa ikinyesha katika kipindi cha siku mbili zilizopita, Kaunti ya Lamu imeharibu barabara ya Pandanguo kuelekea Witu.

Barabara hiyo ya kilomita 21 ndiyo tegemeo la kipekee kwa wakazi wanaoishi kijiji cha Pandanguo, ambao hutumia barabara hiyo kusafirisha chakula kutoka mji wa Witu.

Kijiji cha Pandanguo ambacho ni makazi ya watu wa jamii ya walio wachache ya Waboni hakina maduka wala hospitali.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumanne, wakazi walieleza hofi kwamba huenda wakaumia kwa njaa endapo barabara hiyo haitakarabatiwa kufuatia uharibifu uliochangiwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha eneo hilo.

Msemaji wa wakazi wa Pandanguo, Ali Sharuti alisema imewawia vigumu kwao kutafuta chakula na matibabu kwani barabara yao kwa sasa haipitiki kutokana na matope na maji yaliyotapakaa kila mahali.

“Tunasumbuka tangu mvua ilipoanza kunyesha eneo letu mwanzoni mwa juma hili. Barabara yetu ya Pandanguo-Witu imeharibiwa na mvua na haipitiki. Tumesalia majumbani mwetu. Hatuwezi kufika Witu kujinunulia chakula. Magari pia hayawezi kufika kijijini mwetu kuleta chakula. Serikali ifikirie kuikarabati barabara yetu la sivyo tutaumia kwa njaa,” akasema Bw Sharuti.

Bi Halima Tete aliikashifu serikali kuu kwa kuahidi kujijenga barabara hiyo na kisha kukiuka kutekeleza ahadi hiyo.

Bi Tete alisema jamii ya Waboni imekuwa ikitelekezwa katika huduma nyingi za kiserikali.

Aliwaomba viongozi wa kaunti, ikiwemo, Gavana, Fahim Twaha, Mbunge, Stanely Muthama na wengineo kuiangazia barabara ya Pandanguo-Witu ili ijengwe.

“Tunakosa huduma nyingi, ikiwemo matibabu na hata chakula kutokana na hali mbaya ya barabara yetu. Tungeomba viongozi wetu wasaidie kusukuma ili barabara yetu ikarabatiwa. Tunasumbuka,” akasema Bi Tete.

Kijiji cha Pandanguo kina zaidi ya wakazi 2000.