Habari Mseto

Mvua kubwa yaja, Idara ya Utabiri yaonya

June 5th, 2018 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

MVUA kubwa inatarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, haswa kanda za Bonde la Ufa, Kaskazini na Kati, kulingana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa.

Idara hiyo ilionya kuwa mvua hiyo huenda ikasababisha mafuriko hivyo ikawataka Wakenya kuwa chonjo.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, idara hiyo ilisema mvua hiyo kubwa itanyesha katika kaunti zisizopungua 21.

Kaunti hizo zinajumuisha Turkana, Marsabit, Samburu, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Bungoma na Baringo.

Nyingine ni Nakuru, laikipia, Isiolo, Nyandarua, Kirinyaga, Meru, Tharaka Nithi, Embu, Kiambu, Nairobi, Murang’a na Nyeri.

Idara hiyo pia imeshauri wakazi wa maeneo ya mjini kuwa macho kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mafuriko.

“Wakazi wa maeneo ya mijini wanafaa kuwa macho kuhusiana na uwezekano wa kutokea kwa mafuriko. Jiepushe na maeneo yaliyofurika,” ikasema idara hiyo.

Idara hiyo pia ilionya Wakenya dhidi ya kutembea au kuendesha pikipiki, baiskeli au gari ndani ya maji yanayoenda kwa kasi.

Wakenya pia wametakiwa kuepuka maeneo ambayo hukumbwa na radi mara kwa mara kama vile kujikinga mvua chini ya miti na kuwa karibu na madirisha yaliyo na vyuma.

Wakazi wa maeneo ambayo hukumbwa na maporomoko ya ardhi kama vile Kaunti ya Murang’a wametakiwa kutozuru maeneo hatari.

Watu zaidi ya 100 wameuawa na wengine 260,0000 kusalia bila makao kufuatia mafuriko yaliyoshuhudiwa katika kipindi cha miezi minne iliyopita, kulingana na wizara ya Ugatuzi na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Kaunti 10 ambazo zimeathiriwa zaidi na mafuriko hayo ni Tana River, Kilifi, Garissa, Wajir, Kisumu, Mandera, Isiolo, Turkana, Samburu, Baringo na Kajiado.