Mvua kunyesha nchini Januari 15 hadi 19, yasema idara ya utabiri wa hali ya hewa

Mvua kunyesha nchini Januari 15 hadi 19, yasema idara ya utabiri wa hali ya hewa

Na CHARLES WASONGA

IDARA ya utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya imetangaza kuwa mvua ya kadri itashuhudiwa maeneo mbalimbali kati ya Jumamosi, Januari 15, 2022 na Jumatano, Januari 19, 2022.

Kulingana na ripoti yake ya hivi punde, idara hiyo inasema kuwa mvua kubwa itashuhudiwa katika zaidi ya kaunti 40 ndani ya siku hizo tano.

Ilisema kuwa huenda mvua hiyo ikaandamana na upepo mkali na ngurumo za radi haswa katika kaunti zinazopakana na Ziwa Victoria.

Kando na maeneo ya Ziwa Victoria, mvua itashuhudiwa Magharibi mwa Nyanda za Juu, Kati na Kusini mwa Rift Valley.

Vile vile, mvua hiyo itanyesha katika nyanda za juu mashariki mwa Rift Valley, Nairobi, sehemu kadha za Kaskazini Mashariki, Mashariki mwa Kenya na Pwani.

Jumamosi jioni mvua kubwa ilishuhudiwa katikati mwa jiji la Nairobi na viungani mwake.

Hata hivyo, maeneo kadha Kaskazini Mashariki mwa Kenya yatasalia kavu na hayatashuhudia mvua.

Kaunti za Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Nandi, Trans Nzoia na zile za magharibi kama vile Kakamega, Bungoma, Vihiga na Busia pia zitapata mvua.

Kaunti zote sita za Nyanza kama vile; Siaya, Kisumu, Migori, Kisii, Nyamira na Homa Bay pia zitashuhudiwa mvua ya kiasi cha wastani.

Kaunti zilizoko Mashariki mwa Rift Valley kama vile; Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka na Nairobi, zitapata mvua.

Maeneo mengine yanayotarajiwa kupokea mvua ni kaunti za Mashariki kama vile Makueni, Machakos, Kajiado, Kitui na Taita Taveta. Hii ni sawa na kaunti za pwani kama vile; Mombasa, Tana River, Kilifi, Lamu na Kwale.

Katika muda huo wa siku tano viwango vya joto mchana vinatarajiwa kupanda hadi kati ya nyuzi joto 25 na 28 huku vikishuka usiku hadi kati ya nyuzi joto 13 na 16.

Kwa upande mwingine, kaunti zitakazosalia kavu ni; Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, Isiolo, Turkana na Samburu zitasalia kavu.

You can share this post!

COVID-19: Mechi ya EPL kati ya Tottenham na Arsenal...

UJAUZITO NA UZAZI: Kuongeza madini ya chuma mwilini

T L