Habari Mseto

Mvua yasababisha moto Hospitali Kuu ya Pwani

November 12th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

MTAFARUKU ulizuka kwa muda katika Hospitali Kuu ya Pwani mjini Mombasa, baada ya moto kuzuka kutoka kwa swichi kuu ya hospitali hiyo.

Kulingana na waziri wa Afya katika Kaunti ya Mombasa, Bi Hezel Koitaba, moto huo uliotokea saa mbili asubuhi ulisababishwa na mvua inayoendelea kunyesha,ambayomajiyake yaligusanyaya za umeme.

“Kama mnavyoona kumekuwa na mvua za hapa na pale bila shaka cheche haziwezi kosekana,” alisema Bi Kotaba.

Japo walioshuhudia moto huo walidai kuwa uliathiri shughuli katika chumba cha upasuaji, Mkuu wa usimamizi wa hospitali hiyo, Dkt Iqbal Khandwalla, alisema zilikuwa cheche tu ambazo hazikusababisha maafa yoyote kwa hospitali na wagonjwa.

Alisema moto huo uliteketeza nyaya za swichi kuu iliyoko katika afisi za usimamizi wa hospitali hiyo. Dkt Khandwalla alisema maafisa wa zimamoto kutoka idara ya wazima moto ya Mombasa Kaunti na wale wanaohudumu katika hospitali hiyo walidhibiti cheche hizo kabla ya kusababisha hasara.

“Halikuwa tukio kubwa, tulipogutukia cheche tuliita maafisa wa zimamoto mara moja kama njia ya kuchukua tahadhari ikizingatiwa kuwa sehemu hii inahudumia maelfu ya watu,” alieleza Dkt Khandwalla.

Alisema tayari uchunguzi umeanza kubaini chanzo cha cheche hizo.Kulinga na Bi Margaret Kinyua aliyekuwa ameenda katika hopitali hiyo kuzuru jamaa yake alisema walisikia mlio mkubwa kabla kuona moto ukitokea maeneo ya afisi ya jengo la usimamizi wa hopsitali hiyo.Alisema mlipuko huo uliwafanya wauguzi na baadhi ya wangojwa kukimbilia nje kwa usalama.

“Nilikuwa natoka wadi kusalimia mgonjwa ghafla nikasikia mlio wa mlipuko, kufika nje naona moshi na moto,” alisema Bi Kinyua.Bi kinyua alisema pia walishuhudia giza baada ya umeme kupotea kwa muda.

Alidai pia baadhi ya wagonjwa walikuwa wameanza kuhamishwa kutoka wadi walizokuwa wamelazwa kuepuka maafa kama moto huo ungesambaa.

Madai hayo yalipingwa na waziri Koitaba na msimamizi wa hospitali hiyo Bw Khandwalla wakizitaja kama porojo tu.Wawili hao waliongezea kuwa hospitali hiyo iko na uwezo wa kukabiliana na visa aina hiyo wakisema kuwa wana vifaa vyote vilivyohitajika.

kutoa huduma ya kwanza.“Tuko na mitungi ya gesi inayoweza kuzima moto pindi tu unapoanza, pia kunamaafisa ambao wamepitia mafunzo ya kukabiliana na matukio ya moto na jinsi ya kuokoa,” akasema Bi Koitaba.