Habari Mseto

Mvulana amuua mpenzi wa mamake

March 20th, 2019 1 min read

Na Vitalis Kimutai

MWANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza katika Kaunti ya Kericho alimuua kwa kumdunga kisu mpenzi wa mamake baada ya kuwakuta wakila uroda nyumbani kwao.

Polisi wameanzisha msako kumtafuta mwanafunzi huyo wa Shule ya Upili ya Kaborous ambayo ni ya kutwa.

Habari zilisema alienda mafichoni mara moja baada ya kisa hicho ambacho kilitokea katika kijiji cha Ririat, lokesheni ya Cheborgei, Kaunti Ndogo ya Bureti.

Mwanamume aliyeuawa, ambaye ana umri wa miaka 65, alianguka na kufariki nje ya nyumba alipokuwa akijaribu kutoroka.

Kulingana na jirani, Bi Irene Langat, mvulana huyo, 16, aliingia jikoni ambako mamake ambaye ni mjane alikuwa akijamiana na mwanamume huyo Jumatatu usiku ndipo akamdunga kisu mara kadhaa kifuani.

Mkuu wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Bureti, Bw Ali Abdi alithibitisha kisa hicho.

Babake mvulana huyo alifariki miaka michache iliyopita.