Habari Mseto

Mvulana anayedaiwa kushambuliwa na walinzi wa misitu aaga dunia

May 14th, 2024 1 min read

NA MERCY KOSKEI

MVULANA wa umri wa miaka 16 aliyekuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret baada ya kudaiwa kushambuliwa na maafisa wa Shirika la Misitu nchini (KFS), amefariki.

Stephen Mwangi, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika shule mojawapo katika Kaunti ya Baringo, alikuwa akipokea matibabu katika hospitali hiyo tangu Ijumaa alipolazwa akiwa na majeraha mabaya kichwani na mbavuni.

Inadaiwa Stephen alivamiwa na walinzi wawili wa KFS Jumatano wiki jana alipokuwa akiwazuia kumnyanyasa mama yake kingono katika msitu wa Koibatek.

Lakini walinzi hao badala yake walianza kumpiga na kumjeruhi vibaya.

Kulingana na mamake, Bi Mary Wambui, mwanawe aliaga dunia Jumatatu saa tano usiku akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Alikuwa amelazwa ICU siku mbili zilizopita.

“Tangu Jumatano mwanangu alikuwa hawezi kuzungumza na Jumatatu usiku tulimpoteza. Alilazwa ICU Jumamosi saa mbili usiku kabla ya kuaga dunia Jumatatu,” alisema Bi Wambui.