Habari Mseto

Mvulana auliwa akiwa malishoni na mifugo kuibwa

February 14th, 2024 1 min read

KEVIN MUTAI NA KALUME KAZUNGU

POLISI katika Kaunti ya Kwale wanachunguza mauaji ya mvulana ambaye mwili wake uliokuwa ukioza uligunduliwa msituni Jumanne, siku mbili baada ya kutoweka.

Mtoto huyo, 11, aliondoka nyumbani Jumapili kupeleka mifugo malishoni akiwa na zaidi ya ng’ombe 30 na mbuzi zaidi ya 60.

Polisi kutoka kituo cha Burani kilicho Shimba Hills, walipokea simu kutoka kwa wananchi katika kijiji cha Kirazini ambao waligundua mwili huo.

Wakazi baadaye walipata ng’ombe wote karibu na eneo la uhalifu lakini mbuzi wote hawakupatikana.

Wakati huo huo, watu wasiopungua 20 hufariki huku mali ya mamilioni ya fedha ikiharibika kila mwaka kwa ajali za mashua na maboti Kaunti ya Lamu.

Ripoti kutoka kwa ofisi ya Majanga na Shughuli za Uokozi ya Kaunti ya Lamu inaashiria kuwa ajali nyingi ni zile zinazohusisha vyombo vya baharini vilivyobeba mazao ya mashambani.

Meneja Mkurugenzi wa Idara ya Majanga na Uokozi wa Kaunti ya Lamu, Bw Shee Kupi, alisema ajali hizo mara nyingi zinahusishwa na mabaharia ambao wamekuwa wakitumia vyombo vidogo vya uchukuzi wa baharini ilhali mizigo inayobebwa ni mizito kupita kiasi.

Bw Kupi anasema ni kupitia maamuzi hayo ambapo Lamu imekuwa ikirekodi ajali za baharini, maafa na mali kuangamia kila mara.