Habari Mseto

Simanzi mvulana kufariki akiokoa mbwa wake mtoni

May 31st, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

HALI ya simanzi ilikumba kijiji cha Kirandich, Kuresoi Kusini kaunti ya Nakuru Jumatano wakati mvulana wa umri wa miaka 12 alipozama na kuangamia ndani ya mto Kapkores akijaribu kumwokoa mbwa wake.

Mvulana huyo ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la Saba alijitoma ndani ya mto huo akilenga kumnusurua mbwa wake aliyekuwa akimwandama sungura wa mwituni ndipo akakumbana na mauti.

Mwili wa mvulana huyo baadaye ulipatikana ukielea majini mita kadhaa kutoka eneo la mkasa huo.

Hata hivyo mbwa huyo alinusurika kwa kuogelea nje ya mto huo huku hali ya huzuni ikiwakabili wanakijiji wasiamini mvulana huyo alikuwa ameangamia.

“Tunafikiria kwamba alihofia huenda mbwa wake angefariki majini ndipo akajaribu kumwokoa lakini akateleza na kuzama majini,” akasema Chifu wa eneo hilo Christine Chumo akiongea na waandishi habari kuhusu tukio hilo.

Aidha, Bi Chumo alidai kwamba ilikuwa vigumu kumwokoa mvulana huyo kwa kuwa alisombwa kwa kasi na maji ya mto, mita kadhaa kutoka alikotumbukia majini.

Mwili wa mwendazake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha kaunti ndogo ya Molo.