Habari Mseto

Mvulana tineja ashukiwa kunajisi, kulawiti watoto wanane

April 25th, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

AKIWA na umri wa miaka 14, amekuwa mgeni wa mara kwa mara katika kituo cha polisi si kwa ajili ya kujifunza yanayofanyika kituoni bali kama mshukiwa wa makosa ya ngono.

Mvulana huyo ambaye ni mwanafunzi katika shule moja eneo la Peris katika Kaunti Ndogo ya Ainabkoi anadaiwa kuwanajisi na kuwalawiti watoto wanane katika mtaa wake.

Polisi wanashuku kwamba huenda alianza kujihusisha na uhalifu wa kingono akiwa na umri wa miaka 10.

Miongoni mwa wahasiriwa ni pamoja na marafiki wake ambao hucheza naye hasa wavulana wenye umri wa kati ya miaka mitano na tisa.

Kulingana na polisi mshukiwa ana rekodi ya kuwanajisi wasichana na kulawiti wavulana.

“Kila anapoletwa stesheni tumekuwa tukimuonya na kumwachilia kutokana na umri wake mdogo,” alisema afisa mchunguzi wa kesi hiyo kutoka kituo cha polisi cha Ainabtich wakati wa ombi mbele ya mahakama ya Eldoret la kumzuilia mshukiwa akisubiri uchunguzi wa mojawapo ya kesi hizo.

Afisa wa upelelezi ambaye alizungumza kwa njia isiyo rasmi kortini mbele ya hakimu wa Eldoret, alijuta kuwa juhudi za kumsaidia mvulana huyo kujirekebisha ili kuepusha kupelekwa kortini zimeambulia patupu.

“Hatukutaka kuharakisha suala hilo mahakamani tukikumbuka kuwa ni mtoto anayehitaji kutunzwa na ulinzi lakini kutokana na tabia yake isiyofaa tumelazimika kutumia njia za kisheria kuhusu suala hili,” alisema afisa huyo.

Wiki moja iliyopita, alifikishwa kortini kujibu mashtaka ya makosa ya ngono lakini kutokana na umri wake na aina ya uhalifu husika, Hakimu Mkazi Mkuu wa Eldoret, Kyne Odhiambo, aliamuru mtoto huyo asaidiwe kupata wakili wa kujitolea kabla asomewe mashtaka.

Amekuwa akizuiliwa katika kituo cha kurekebisha tabia cha Eldoret Rescue Centre.

Baada ya kutafuta wakili wa kujitolea, alishtakiwa Jumatatu kwa kumlawiti mvulana wa umri wa miaka tisa.

Shtaka lilisema kuwa mnamo Machi 23, 2024, katika mtaa wa Peris eneo la Kimumu katika Kaunti Ndogo ya Ainabkoi, alimlawiti mvulana wa umri wa miaka tisa kinyume na kifungu cha 8 cha sheria ya makosa ya ngono ya 2006.

Alikanusha shtaka hilo.

Kutokana na umri wake, mahakama ilimruhusu mamake kulipa Sh8,000 kama dhamana ya pesa taslimu ili kuachiliwa huru akisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hiyo.

Kesi hiyo itatajwa Mei 3, 2024.