Mvutano baina ya Ingwe na FKF kuhusu debi ya Mashemeji

Mvutano baina ya Ingwe na FKF kuhusu debi ya Mashemeji

Na CECIL ODONGO

UONGOZI wa Klabu ya AFC Leopards umesisitiza kwamba mchuano mkali wa debi kati yao na mahasimu wao wa tangu jadi Gor Mahia utaendelea Jumapili hii katika uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Katibu Mkuu Oscar Igaida alipuuzilia mbali kauli ya Rais wa Shirikisho la soka nchini (FKF) Nick Mwendwa kwamba mechi hiyo iratibishwe upya ili kupisha michuano ya kirafiki wiki kesho kati ya Timu ya Taifa Harambee Stars na mataifa ya Uswazi na Equitorial Guinea.

“Hatutawachilia wachezaji wetu washiriki katika mechi za timu ya taifa kutokana na mechi ya debi na ile ya kombe la supa Tarehe 3 mwezi Juni mwaka 2018,” akasema Bw Igaida.

Aidha katibu huyu alikashifu matamshi yanayodaiwa kutolewa na Bw Mwendwa kwamba debi ya mashemeji haifai kusakatwa kwenye uwanja wa ‘kiajabu’ kama Bukhungu.

“Ni kinaya kikubwa kwa Bw Mwendwa kudai kwamba uwanja wa Bkhungu ni wa kiajabu. Kwani wakati wakiandaa mechi za CECAFA hapo mwaka 2017 hawakujua ni wa kiajabu?” ikasema taarifa ya Bw Igaida.

Bw Igaida alisisitiza kwamba wataendelea na matayarisho kabambe kwa ajili ya mchuano wa debi na hawataruhusu wachezaji wao washiriki mechi za kirafiki ambazo hazipo kwenye kalenda ya Shirikisho la soka duniani (FIFA).

Mapema leo, Bw Mwendwa alisema kwamba debi hiyo ya Tarehe 26 mwezi Mei mwaka 2018 hautachezwa wala uwanja wa Bkhungu hautatumika kuandaa kipute hicho.

You can share this post!

Mugabe aitwa bungeni kufichua yalikoenda mabilioni ya almasi

Misikiti yaagizwa ipeperushe bendera, ifunze waumini kuhusu...

adminleo