Habari

Mvutano baina ya TSC na Knut washuhudiwa katika kongamano Mombasa

December 4th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

VITA baina ya chama cha walimu (Knut) na Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC) vimejitokeza katika kongamano la 15 la walimu wakuu wa shule za msingi linaloendelea Mombasa.

Jumatatu maafisa wa TSC waliamua kutoka katika kongamano hilo baada ya Katibu Mkuu wa Knut Wilson Sossion kuhudhuria kongamano bila mwaliko na kuhutubia walimu zaidi ya 7,000.

Kulingana na afisa mmoja wa Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (Kepsha) ambaye hakutaka kutajwa jina, ni kwamba baada ya Bw Sossion kuhutubia, maafisa wa TSC walimuendea mwenyekiti Kepsha Bw Nicholas Githemia na kudadisi ni kwa nini katibu huyo alipewa fursa hiyo.

“Maafisa wa TSC walimtaka Bw Githemia kumfurusha Sossion jukwaani kwa kuwa hakuwa amealikwa kuhudhuria kongamano,” alieleza.

Nayo Jumatano afisa mkuu mtendaji wa TSC Dkt Nancy Macharia alitarajiwa kuhudhuria kongamano hilo ambalo linaendelea katika chuo cha serikali cha kutoa mafunzo ya ushuru lakini hakufika.

Mdokezi amedai kuwa Dkt Macharia hakuhudhuria kufuatia kuruhusiwa kwa Bw Sossion kuhutubia walimu bila ya mwaliko.

Katika hutuba yake Bw Sossion alipinga sera mpya za serikali kuhusu ugavi wa vitabu shuleni na akakosoa hatua ya serikali kuhamisha walimu kutoka kauntu moja hadi nyingine.

Uwazi

Aidha Bw Sossion aliwaomba walimu kusalia kuwa kitu kimoja, na kukumbatia demokrasia na mazungumzo katika kusuluhisha migogoro.

“Vita dhidi yangu vilikuwa ni mbinu ya kuvunja muungano wa walimu. Nataka kuwahakikishia kuwa hakuna mtu atakayening’atua katika kiti hiki. Serikali pamoja na tume ya kuajiri walimu nchini TSC waache kutuvurugia shughuli zetu,” alifoka Sossion.

Kulingana na walimu hao muungano huo unapigwa vita na watu wan je na hata baadhi ya walimu.

Punde tu maafisa walipoingia katika ukumbi wa chuo hicho walimu walianza kuimba nyimbo za umoja na kulazimisha Kepsha kuwapa maafisa hao nafasi kuhutubia walimu wakuu.

Wakati huo huo waliomba ushirikiano wa walimu katika kuzungumzia masuala muhimu yanayoathiri sekta ya elimu.