Habari MsetoSiasa

Mvutano bungeni Keter akikataa kujibu maswali kuhusu mradi wa Sh74b

March 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KULITOKEA majibizano makali katika kamati moja ya seneti Jumatano adhuhuri pale Waziri wa Kawi Charles Keter alipokataa kujibu masuali kadhaa kuhusu Mradi wa Kuzalisha Kawi kutokana na Upepo, (Lake Turkana Wind Power Project) katika kaunti ya Marsabit. Mradi huo unagharimu Sh74 bilioni.

Alisema alipata ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu Paul Kihara kwamba asizungumzie suala hilo kutokana na kesi mbili kulihusu zilizoko mahakamani.

Bw Keter aliiambia Kamati ya Seneti kuhusu Kawi hivi: “Sijakataa kujibu swali lolote. Lakini nimeshauriwa na Mwanasheria Mkuu ambaye ndiye mshauri wa serikali katika masuala ya sheria, kwamba suala hilo liko kortini. Hata hivyo, sina cha kuficha na nilikuwa tayari kabisa kutoa ufafanuzi wote.”

Maseneta walikerwa na usemi huu huku wakidai kuwa anajifucha nyumba kesi iliyo kortini ili kukwepa kuwajibikia suala hilo linalohusi wizara yake.

“Maswali yaliyoibuliwa kuhusu mradi huu hayataingilia au kuathiri shughuli za korti ya kisheria. Hakuna shughuli za kortini zinazoweza kusimamisha uchunguzi kuhusu suala lenye umuhimu wa kitaifa na unaoguzia masilahi ya Wakenya,” akasema Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Kauli ya Bw Wetang’ula iliungwa mkono na mwenzake wa Narok Ledama Ole Kina aliyetaja uamuzi wa Maspika wa Bunge wa hapo awali kuhusu suala kama hilo, maamuzi ambayo walisema yanalipa bunge uwezo wa kuchunguza masuala yaliko kortini “bila kuingilia au kushawishi kesi husika,”

Ole Kina alimwambia Bw Keter kwamba maswlali yaliyoibuliwa kuhusu mradi huo hayawezi kuingilia kesi zilizoko kortini.

Mwaka jana mwanaharakati Okiya Omtata aliwasilisa kesi kortini akitaka kuzuia Wizara ya Kawi kutoa malipa zaidi kwa kampuni ya Lake Turkana Wind Power Ltd, akidai kampuni hiyo ilikuwa imepokea Sh39 bilioni licha ya kutosambaza kawi yoyote.

Bw Keter aliitwa kufika mbele ya kamati hiyo ya Kawi inayoongozwa na Seneta wa Nyeri Ephraim Maina, kutoa ufafanuzi baada ya Bw Wetang’ula kuwasilisha swali katika Seneti akitaka kujua kuhusu thamani ya mradi huo.

Vile vile, maseneta walipendekeza mradi huo kufanyiwa ukaguzi kubaini ni kwa nini kampuni ya Lake Turkana Wind Power Ltd ilipewa kandarasi na Kampuni ya kusambaza umeme nchini, Kenya Power, mnamo 2015 kuzalisha megawati 300 y umeme, ilhali haikutoa hudum yoyote.

Pia maseneta walitaka kujua ikiwa mkataba kati ya kampuni hiyo na Kenya Power ya kuwasilisha nguvu za umeme katika hifadhi ya kitaifa (National Grid) ulikiukwa na Lake Turkana Wind Power Ltd.

Baada ya vuta nikuvute iliyodumu kwa dakika 30 kati ya maseneta na Waziri Keter, mwenyekiti wa Kamati hiyo Seneta Maina aliamuru mapumzika ya dakika tano kutoa nafasi kwa wanachama wa kamati yake kushauriana kuhusu mwelekeo kuhusu suala hilo.

“Suala hili liendelee kushughulikiwa kwa kuwa kesi zilizoko mahakama haziwezi kuzuia kazi ya kamati hii,” seneta Maina akasema.

Lakini Bw Keter alishikilia msimamo wake wa awali kwamba hangejibu maswali hayo baada ya kushauriwa na Mwanasheria Mkuu Bw Kihara kutofanya hivyo.

Hapo ndipo wanachama wa Kamati hiyo waliamua kulegeza msimamo na kumwagiza Bw Keter kurejea Jumatatu wiki ujao akiwa amejpanga kujibu masuali hayo “bila kuingilia kesi iliyoko mahakamani”

“Enda ukashauriane na Mwanasheria Mkuu tena kuhusu namna utakajibu maswali tisa kuhusu suala hili. Tunga majibu yako upya kwa njia ambayo inafikiri haitaingilia kesi hiyo. Lakini ujue kuwa sisi kama Seneti hatuwajibiki kwa Mwanasheria Mkuu,” akasema Bw Maina.

Keter alikubaliana na ushauri huo na kukubali kufika mbele ya Kamati hiyo Jumatatu saa nane na nusu mchana katika majengo ya bunge, Nairobi..