Habari

Mvutano katika seneti hatima ya Waititu ikijadiliwa

January 21st, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SIASA za mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ ndani ya Jubilee zimeshamiri Jumanne katika Bunge la Seneti katika kikao maalum kilichoitishwa kujadili madai yaliyoko kwenye hoja ya kumwondoa afisini Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu Baba Yao.

Baadhi ya maseneta wa chama hicho tawala walipinga majina ya wawakilishi wao katika kamati maalum ya wanachama 11 iliyobuniwa kuchunguza madai dhidi ya Waititu.

Wakiongozwa na kiranja wa wengi Seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata, walidai kuwa kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen aliteua wanachama wa mrengo wa ‘Tangatanga’ pekee katika kamati hiyo huku upande wa ‘Kieleweke’ ukikosa uwakilishi.

“Mheshimiwa Spika, uteuzi wa wanachama wa upande wa walio wengi hauwakilishi na haukufanywa kwa usawa. Sitaunga mkono orodha hii kwa sababu sura ya kamili ya Jubilee haijawakilishwa hapa,” akasema Bw Kang’ata.

Nao maseneta Samuel Poghisio (Pokot Magharibi) na Farhiya Ali (Seneta Maalum) walidai Bw Murkomen aliandaa orodha hiyo kwa lengo la kumwokoa Waititu.

Kwenye orodha ya wanachama 11 iliyosomwa na Bw Murkomen, upande wa Jubilee unawakilishwa na kiranja wa wengi Susan Kihika (Nakuru), Sylvia Kasanga (Seneta Maalum), Hargura Godana (Seneta Maalum), Aaron Cheruiyot (Kericho), Anuar Oloitipitip (Lamu) na Mithika Linturi (Meru).

Na katika mrengo wa upinzani, unawakilishwa na; Cleophas Malala (Kakamega), Mohamed Faki (Mombasa), Oman Farhada (Seneta Maalum), Fred Outa (Kisumu) na Okong’o Omogeni (Nyamira).

Bw Malala alipendekezwa kuwa mwenyekiti huku naibu wake akiwa Bi Kihika.

Nao maseneta Samuel Poghisho (Pokot Magharibi) na Bi Farhiya Ali (seneta maalum) walidai kuwa Bw Murkomen aliteua wanachama wa Tangatanga pekee kwa lengo la kumnusuru Bw Waititu.

“Hatuwezi kukubaliana na orodha hii kwa sababu ilitayarishwa kwa lengo la kuokoa mtuhumiwa. Mashauriano hayakufanyika kabla ya majina haya kuwasilishwa katika kikao hiki,” akalamika Seneta Ali.

Hata hivyo, baada ya mjadala mkali orodha hiyo iliidhinishwa na kamati hiyo kupewa muda wa siku 10 kushughulikia suala hilo kisha iwasilishe ripoti katika kikao cha bunge lote.

Katika hoja iliyopitishwa Desemba 19, 2019, madiwani wa Kaunti ya Kiambu walimsuta Bw Waititu kwa kukiuka Katiba, Sheria za serikali ya kaunti, Sheria kuhusu Ununuzi na Uuzaji wa Bidhaa na Huduma za Umma na Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma.

Gavana huyo amezuiwa kuingia afisini kutokana na kesi ya ufisadi inayomkabili.