Mvutano kuhusu fidia kikwazo kwa mradi wa Sh36 bilioni Pwani

Mvutano kuhusu fidia kikwazo kwa mradi wa Sh36 bilioni Pwani

NA SIAGO CECE

TATIZO la umiliki wa ardhi katika kaunti za Pwani sasa unatishia kukwaza utekelezaji wa mojawapo ya miradi mikubwa inayonuiwa kumwachia sifa Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu.

Ujenzi wa Sehemu Maalum ya Kiuchumi ya Dongo Kundu (SEZ), Kaunti ya Kwale, upo hatarini kugonga mwamba kutokana na mvutano kuhusu fidia.

Wananchi walioathiriwa na mradi huo wamelalamikia kucheleweshwa kwa fidia ili wahame kutoa nafasi ya mradi huo.

Ujenzi wa sehemu hiyo inayolenga ardhi ya ekari 3,000 katika Kaunti za Mombasa na Kwale bado haujaanza kwani wakazi hawajahama makazi yao.

Mradi huo unaokadiriwa kugharimu Sh36 bilioni unanuiwa kuboresha uwekezaji katika Kaunti ya Mombasa na Pwani kwa jumla, kwa kukuza sekta ya kiviwanda na kutoa nafasi za ajira kwa wenyeji.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka inayosimamia SEZ nchini, Dkt Meshak Kimeu, alisema kuna uwezekano wa kusimamisha maendeleo yote yaliyopangwa katika ardhi inayolengwa ikiwa changamoto zinazoibuka hazitatatuliwa.

“Ikiwa wakazi hawajalipwa fidia, miradi mingi ambayo tunapanga kufanya hapa haitawahi kuanza. Makazi mapya ya watu walioathiriwa ni muhimu sana kujengwa kwa hivyo asasi husika za serikali zinafaa kuharakisha ili tupate ardhi ya kufanyia ujenzi,” Dkt Kimemia alisema.

Alikuwa akizungumza na maafisa wakuu wa serikali waliokuwa katika Kaunti ya Kwale kukagua miradi tofauti ya serikali ya kitaifa wiki iliyopita.

Katibu Mkuu wa Ustawishaji Viwanda, Bw Kirimi Kaberia alisema tatizo lililopo ni kuwa wanaodai kuwa wamiliki wa ardhi ni maskwota na hawawezi kulipwa fidia za ardhi.

Kulingana naye, ardhi hiyo ni ya Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) na wakazi wanaotaka fidia hawana hatimiliki.

“Fidia itakayolipwa itakuwa ni kwa mali zao tu kama vile biashara, nyumba na wala si ya kugharamia ardhi. Ardhi tayari ni mali ya serikali. Serikali haiwezi kununua ardhi yake,” Bw Kaberia alisema.

Aliongeza kuwa Sh1.4 bilioni zinahitajika kwa ajili ya malipo hayo ya fidia. Mradi huo ulifaa kukamilika mwaka ujao.

Kando na viwanda, eneo hilo la Dongo Kundu limenuiwa kuwa kituo kikuu cha biashara ya utalii, uchukuzi na ujenzi itakayowezesha wakazi kupata ajira kutokana na wawekezaji wanaotarajiwa kuanzisha biashara zao hapo.

  • Tags

You can share this post!

OKA hatarini kusambaratika vinara wakimenyania tiketi ya...

Raila kifua mbele Pwani akiungwa mkono na magavana watano

T L