Mvutano mitandaoni baada ya Raila kutumia gari la serikali

Mvutano mitandaoni baada ya Raila kutumia gari la serikali

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kutumia gari lenye nambari ya usajili ya serikali alipowasilisha Migori Jumapili imeibua gumzo mitandaoni.

Ingawa Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed amethibitisha kuwa gari hilo ni lile yeye hutumia kutokana na cheo chake cha kiranja wa wachache, Mbunge wa Soy Caleb Kositany alikuwa na wazo tofauti.

Kupitia ujumbe katika akaunti yake ya Twitter Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais William Ruto Jumatatu alisema kuwa kwa kutumia gari la serikali “Raila ameanza kutumia mali ya serikali kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.”

“Hii ndio matunda ya handisheki. Sasa ODM iko seriakali kabisa. Tizama gari analolitumia,” akaandika Kositany na kuweka picha ya gari hilo kando na maandishi hayo.

Akaongeza; “Raila sasa ameanza kupewa mali ya serikali atumie katika kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022. Si hii ni ubadhirifu wa mali ya serikali?”

Lakini Junet alijibu haraka kwa kusema kuwa gari hilo, ambalo Odinga alisafiria alipomtembelea nyumbani kwake, ni ile aliyopewa kwa matumizi yake kama Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa.

“Hilo gari lenye nambari ya usajili ya serikali, GK lilikuwa langu, nilipewa na bunge kutokana na hadhi yangu kama Kiranja wa Wachache. Raila alikuwa akija nyumbani kwangu na nilitumia gari hilo kumsafirisha baada yake kutua kaunti ya Migori kwa helikopta,” Junet akasema kwenye taarifa fupi.

Kulingana na kanuni za bunge, wabunge walioteuliwa kuongoza pande mbili ( upande wa wengi na ule wa wachache) hupewa magari ya serikali na Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Wao ni; Kiongozi wa Wengi na naibu wake na Kiranja wa wengi na naibu wake. Kiongozi wa Wachache na naibu wake na Kiranja wa Wachache na naibu wake.

Kando na hayo wabunge hao hupewa afisi za kifahari katika majengo ya bunge na walinzi zaidi ikilinganishwa na wabunge wengine wasioshikilia nyadhifa zozote za uongozi bungeni.

Hata hivyo, kauli ya Bw Kositany iliendelea kuibua hisia mseto miongoni mwa watumiaji mtandao wa twitter.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Barack Muluka akasema: “Ikiwa Raila anafurahi na kutulia kwa kutumia gari la GK, basi hatupasi kugeuza suala hilo kuwa la mjadala. Tujadili mambo muhimu kwa Wakenya,”

Hata hivyo, mtaalamu kwa masuala ya uongozi Nafula Kisiang’ani alisema kuwa ukuruba wa Bw Odinga na serikali na hatua yake ya kutumia rasilimali za umma ni sehemu ya mkakati wa kumwezesha kumrithi Rais Kenyatta mwaka wa 2022.

You can share this post!

Kenya yamaliza mkiani voliboli ya kinadada Olimpiki

Itumbi sasa aililia korti baada ya kudai kulikuwa na njama...