Mvutano wa kuvunja serikali ya Vihiga waendelea

Mvutano wa kuvunja serikali ya Vihiga waendelea

Na DERICK LUVEGA

JUMLA ya wapigakura 55,000 wa Vihiga wametia sahihi zao katika ombi la kutaka serikali ya kaunti hiyo ivunjwe, huku uongozi wa ODM eneo hilo ukitaka chama hicho kiingilie kati kutatua mzozo huo.

Mpango huo ulianzishwa na aliyekuwa Katibu wa Kaunti hiyo Francis Ominde na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Joseph Simekha, ambao ni wandani wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga.Wawili hao wanataka serikali ya kaunti hiyo, inayoongozwa na Gavana Wilbur Otichillo, ivunjwe kwa misingi ya makosa sita yakiwemo madai ya ufisadi, matumizi mabaya ya ofisi na utepetevu.

Baada ya kupatikana kwa sihihi hizo, sasa macho yanaelekezwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye atahitajika kuidhinisha au kukataa ombi hilo.Kwa hofu kwamba hatua hiyo itaathiri kaunti hiyo, Mwenyekiti wa ODM tawi la Vihiga, Zebedee Osabwa alisema amewasiliana na makao makuu ya chama hicho ili kizime mipango hiyo.

Gavana Otichillo, kupitia tawi la ODM kaunti ya Vihiga, anautaka uongozi wa chama hicho kudhibiti wapangaji wa mikakati ya kuvunja serikali yake.Tayari Bw Osabwa amewasilisha ombi kwa Mwenyikiti wa ODM, John Mbadi na Katibu Mkuu Edwin Sifuna akiwataka waingilie kati.

Lakini jana, Bw Simekha alifafanua hatua yake haijachochewa wala kudhaminiwa na ODM, akisema ni wananchi wa Vihiga ambao wameanzisha mchakato huo“Wananchi kutoka vyama mbalimbali ndio wanaendesha mchakato huo unaolenga kusafisha kaunti ya Vihiga,” akaeleza.

Bw Simekha alisema chama cha ODM hakitakubali kujiingiza katika mchakato huo ulioanzishwa na wananchi kwa nia ya kuondoa maovu yanayowakosesha huduma.

You can share this post!

Covid yalipuka Kisumu wiki baada ya ziara ya Uhuru, Raila

Karo: Magoha ataka watoto wafukuzwe