Habari MsetoSiasa

Mvutano wa Uhuru, Ruto watatiza kikao cha kumtimua Waititu

January 21st, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SIASA za mirengo ya Tangatanga na Kieleweke ndani ya Jubilee zilijitokeza wazi jana katika Bunge la Seneti wakati wa kikao maalum kilichoitishwa kujadili hoja ya kuamua mbinu ya kusikiza hoja ya kumwondoa ofisini Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu.

Baadhi ya maseneta wa chama hicho tawala walipinga majina ya wawakilishi wao katika kamati maalum ya wanachama 11 iliyokuwa imependekezwa.

Baada ya vuta nikuvute kuhusu uanachama wa kamati hiyo maalum, maseneta waliamua kwamba suala hilo lishughulikiwe na kamati ya bunge lote.

Maseneta 28 walipiga kura ya kuunga mkono suala lisikizwe katika kamati ya wote huku 11 wakiunga mkono kamati.

Kwenye mjadala kuhusu majina ya wanachama wa kamati iliyokuwa imependekezwa, baadhi wakiongozwa na kiranja wa wengi, Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a, walidai kuwa kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen aliteua wanachama wa mrengo wa Tangatanga pekee katika kamati hiyo.

Nao maseneta Samuel Poghisho (Pokot Magharibi) na Farhiya Ali (seneta maalum), walisema orodha hiyo ililenga kumnusuru Gavana Waititu kwa sababu inajumuisha wanachama wengi wa Tangatanga.

Katika orodha ya watu 11 iliyopendekezwa na Bw Murkomen, upande wa Jubilee ungewakilishwa na naibu kiranja wa wengi Susan Kihika (Nakuru), Sylvia Kasanga (Maalum), Hargura Godana (Maalum), Aaron Cheruiyot (Kericho), Anuar Oloitipitip (Lamu) na Mithika Linturi (Meru).

Nao mrengo wa upinzani ulikuwa uwakilishwe na Cleophas Malala (Kakamega), Mohamed Faki (Mombasa), Oman Farhada (Maalum), Fred Outa (Kisumu) na Okong’o Omogeni (Nyamira).