Habari Mseto

Mvutano wanukia Mombasa serikali ikipanga kuzima madereva, utingo ‘kuchonga’ miraa

May 20th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa inapanga kuweka sheria kali zaidi kuepusha uraibu wa utafunaji miraa na muguka hasa miongoni mwa watoto.

Gavana Abdulswamad Nassir, amesema baadhi ya sheria hizo ni kwamba, madereva na wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma yakiwemo tuktuk na bodaboda watapigwa marufuku kutafuna miraa na muguka wakiwa kazini.

Kulingana naye, hii inalenga kuepusha matumizi ya bidhaa hizo mbele ya watoto wadogo. Vilevile, alisema magari ya umma yatapigwa marufuku kusafirisha bidhaa hizo bila leseni.

Kulingana na kiongozi huyo, uraibu wa miraa na muguka umechangia utovu wa nidhamu, uhalifu na utovu wa maadili miongoni mwa wanafunzi ambao wengine hata wameacha shule.

Bw Nassir alisema serikali yake itatenga sehemu pa kuuzia miraa na muguka ili wanafunzi wasiuziwe matawi hayo hatari kwa afya yao.

“Mkitaka kusafirisha mizigo hiyo chukueni leseni, hatutakubali mchanganye miraa, muguka na abiria. Wafanyabiashara wa miraa na muguka pia watalazimika kuchukua leseni ya biashara hiyo,” alisema Bw Nassir.

Alisema ameshawaandikia barua wamiliki wote wa mabasi kuanza kufuata agizo hilo.Maduka yanayouza miraa na muguka karibu na taasisi za elimu, makanisa na misikiti tayari yameanza kufungwa.

Bw Nassir alisema maduka hayo yanafaa kuwa umbali wa mita 100 kutoka sehemu za kuabudu pamoja na taasisi za elimu.

Ameshikilia msimamo wake kudhibiti biashara ya miraa na muguka licha ya shinikizo kutoka kwa wanasiasa wa Meru na Embu kulinda biashara hiyo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Gavana wa Embu, Cecily Mbarire na Seneta wa Meru Kathuri Murungi, wanasiasa wengine na wafanyabiashara wa miraa na muguka kuendelea kumiminika Mombasa kumsihi Gavana Nassir kutuliza msimamo wake, hasa kuhusu kuongeza ada ya kufanya biashara hiyo.

Kwenye Mswada wa Fedha wa 2024, Serikali ya Gavana Nassir imeongeza ada ya kusafirisha muguka kutoka kunakokuzwa hadi Mombasa kwa kutoza Sh80,000 kwa kila tani saba kutoka Sh24,000 iliyokuwa ikitozwa hapo awali.

“Kwanza ningekuwa na uwezo ningepiga marufuku muguka. Ina madhara mabaya sana kwa watoto wetu ambao baada ya kutafuna wanaanza kufanya mambo ya kiajabuajabu. Kwa sasa kuna waraibu 76 wa mihadarati waliolazwa katika Hospitali ya wagonjwa wenye matatizo ya akili ya Port Reitz, 45 kati yao wakiwa waraibu sugu wa muguka,” alisema Bw Nassir.

Viongozi wengine wa Mombasa wakiwemo madiwani, wabunge Mohammed Machele (Mvita), Badi Twalib (Jomvu), Omar Mwinyi (Changamwe), Rashid Bedzimba (Kisauni) na Mbunge Mwakilishi wa Kike Zamzam Mohammed wamekuwa wakilalamika kuhusu utafunaji wa matawi hayo ya miraa na muguka miongoni mwa wanafunzi.

Vilevile, viongozi wa kidini na wadau wa elimu wamekuwa wakishinikiza bidhaa hizo zipigwe marufuku kabisa jijini Mombasa. Seneta Murungi alisema wafanyabiashara wa miraa wanakadiria hasara kubwa kutokana na kuongezwa kwa ada ya usafirishaji.

“Miraa imekuwa ikiuzwa hapa Mombasa kwa miaka na mikaka na haijawahi kumdhuru mtu yeyote, hata tunashangaa yanayojiri kwa sasa. Miraa ni mmea unaopewa heshima kubwa sana kule kwetu hata inatumika kwenye malipo ya mahari,” alieleza.