Mvuvi afariki Lamu mawimbi makali yakiendelea kuyumbisha vyombo vya baharini

Mvuvi afariki Lamu mawimbi makali yakiendelea kuyumbisha vyombo vya baharini

NA KALUME KAZUNGU

MVUVI mmoja amefariki na wengine wawili kunusurika kifo pale mashua walimokuwa wakisafiria ilipolemewa na mawimbi makali na kuzama baharini kwenye kivuko cha Mlango wa Tanu, karibu na Kiwayu kaunti ya Lamu Jumanne.

Ajali hiyo ilitokea saa moja na nusu asubuhi, huku kaunti za Pwani zikiendelea kushuhudia upepo mkali tangu Jumatatu.

Akithibitisha ajali hiyo, Afisa Mkuu wa Idara ya Majanga ya Dharura wa kaunti ya Lamu, Shee Kupi, alisema aliyefariki ni Araphat Mohamed Kombo, 29.

Wavuvi wengine wawili, Mohamed Zedi, 35 na Mohamed Mbwana,44, walifaulu kuogelea hadi nchi kavu punde mashua yao ilipozama.

“Leo majira ya asubuhi wavuvi watatu walizama baharini baada ya mashua yao kusombwa na mawimbi makali baharini eneo la Mlango wa Tanu huko Kiwayu. Wawili walijitahidi kuogelea hadi nchi kavu lakini mmoja wao, Araphat Mohamed Kombo, akashindwa na nguvu, hivyo kufa maji baharini. Tayari mwili wake umepatikana hivi adhuhuri na mazishi yake yamefanyika,” akasema Bw Kupi.

Ajali hiyo inajiri siku moja baada ya idara ya hali ya anga nchini kutoa onyo kwa wavuvi na mabaharia wengine, hasa kwenye Bahari Hindi kaunti za Kwale, Mombasa, Kilifi na Lamu kuepuka kusafiri au kutekeleza shughuli zao kwenye baharini ya kina kirefu ili kuepuka ajali na maafa.

 

  • Tags

You can share this post!

Obiri atupia jicho mbio za mita 5000 baada ya kutamba...

Harakati za utoaji chanjo ya HPV nchini zasuasua

T L