Habari Mseto

Mvuvi aliyefariki akisubiria fidia ya Lapsset

April 19th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

KISA ambapo mvuvi alikufa maji katika Bahari Hindi eneo la Lamu mnamo Jumatano, kimeibua upya wito wa wavuvi kulipwa fidia zao na serikali haraka iwezekanavyo.

Hii ni baada ya kubainika kuwa, mvuvi huyo, Bw Sombwana Mohamed Omar, 44, alikuwa mmoja wa wavuvi waliopigania sana fidia ya Sh1.76 bilioni kufuatia athari za ujenzi wa Bandari ya Lamu (LAPSSET) na pia alifaa kulipwa fidia hiyo.

Alifariki wakati mashua walimokuwa wakitekelezea uvuvi kwenye Bahari Hindi ilipozama baada ya kukumbana na upepo mkali eneo la Kipungani.

Mwenyekiti wa Miungano ya Wavuvi (BMUs) Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Somo, alithibitisha kwamba Bw Omar alikuwa miongoni mwa wavuvi 4,102 wanaosubiri fidia yao waliyoahidiwa italipwa mwezi huu.

Kulingana na Bw Somo, marehemu pia alikuwa mwenyekiti wa Muungano wa Wavuvi wa Kiongwe Mjini (BMU) ambao una wanachama 18.

Muungano huo unatarajiwa kupata mgao wa Sh4.4 milioni kwa hivyo kila mvuvi katika muungano huo alitarajia kupokea Sh241,700.

“Amesimama na sisi kuisukuma serikali kutulipa fedha zetu za fidia ambazo tumengoja kwa miaka saba sasa. Twasikitika kugundua kuwa Omar amefariki kabla ya kupokea mgao wake,” akasema Bw Somo.

Marehemu ni baba wa watoto watano, wakiwemo pacha wa miaka miwili unusu na kitinda mimba mwenye umri wa miezi mitano.

Kulingana na dadake mdogo, Bi Zuena Mohamed, marehemu alikuwa mtu wa bidii na aliyejitolea kuhakikisha ana kimu vilivyo familia yake kupitia kazi hiyo ya uvuvi.

“Kakangu na sote kama familia tulikuwa na matarajio makubwa ya maisha yetu kubadilika punde tukipata fedha hizo za fidia. Ni masikitiko kwamba amefariki kabla atimize malengo yake,” akasema Bi Mohamed.

Kulingana na takwimu kutoka kwa ofisi ya miungano ya wavuvi Lamu, kifo cha Bw Omar juma hili kimezidisha idadi ya zaidi ya wavuvi 300 wa Lapsset ambao tayari wamefariki wakisubiri fidia yao.

Wiki iliyopita, wavuvi zaidi ya 400 walikusanyika kwenye makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lamu mjini Mokowe, ambapo walitia sahihi makubaliano ya serikali kutoa fedha hizo za fidia mwezi huu.

Mnamo Mei, 2018, Mahakama Kuu mjini Malindi iliamuru Serikali Kuu kuwalipa wavuvi zaidi ya 4,000 wa Lamu kima hicho cha Sh1.76 bilioni kama fidia.

Hii ni baada ya mahakama kupata kuwa mradi wa bandari ya Lamu (Lapsset) ni kweli ulisababisha athari kubwa, ikiwemo kuharibu maeneo ambayo tangu jadi yalikuwa yakitegemewa na wavuvi wa Lamu.