Habari Mseto

Mvuvi auawa na mkewe

October 21st, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MVUVI aliuawa na mkewe wakati wa sikukuu ya Mashujaa alipodugwa kisu katika eneo la Kasarani mjini Naivasha baada ya kuzozana.

Naibu wa Kamanda wa Kaunti, Mbogo Mathioya amesema haikubainika kilichosababisha mwanamke huyo kuyachukua maisha ya mumewe.

Mvuvi huyo, Mathioya amesema alipelekwa zahanati iliyokaribu lakini akatangazwa ameaga punde tu alipofikishwa na wasamaria wema.

“Wawili hao walizozana kabla ya mwanamke huyo kujihami na kisu na kumfuma mumewe kifuani,” amesema mtawala huyo.

Mwanamke huyo alitiwa nguvuni baada ya kisa hicho na anaendelea kuhojiwa na polisi.

Mkazi wa eneo hilo, Joseph Mwaura Kajesh, akizugumza na Taifa Leo amesema wanandoa hao wamekuwa wakizozana tangu wafunge pingu za maisha.

“Wawili hawa wamekuwa wakiishi maisha ya kuvumiliana na mzozano tangu waoane,” amesema Bw Kajesh.

Mwili wa marehemu umepelekwa mochari katika hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha kufanyiwa upasuaji