Habari Mseto

Mwaani Girls yang’aa kwenye mashindano ya kitaifa ya uigizaji

April 8th, 2018 2 min read

Na ANTHONY NJAGI

MTAALA mpya ni miongoni mwa masuala yaliyonaswa katika Tamasha la Kitaifa la Michezo ya Kuigiza na Filamu yanayoendelea jijini Nairobi.

Shule ya Upili ya Wasichana ya Mwaani kutoka Kaunti ya Makueni ilionyesha filamu kwa jina “Juda” iliyotayarishwa na Joan Muchina.

Katika filamu hiyo, mwalimu wa Drama Bi wambua na kundi lake wameshinda shindano la eneo, lakini shuleni kuna shida.

Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Mwaani Girls wakikariri shairi lao ”Krismasi’ kuhusu usalama barabarani lililoandikwa na Joan Muchina katika Tamasha za Mashindano ya Uigizaji zilizoandaliwa katika Shule ya Upili ya Meru Machi 17, 2018. Picha/ Anthony Njagi 

Mzazi ambaye pia ni mwalimu wa somo la Fizikia, hana imani na mambo mengine yanayohusisha talanta kama uigizaji, uogeleaji, uanahabari na kadhalika, isipokuwa elimu na anapinga michezo ya kuigiza kama ya kupoteza wakati.

Tamasha hilo la 59 linaloendelea katika Shule ya Upili ya Lenana linahusisha densi, simulizi na mashairi ya kuigizwa.

Shule ya Set Green Hills Academy kutoka Kisii, iliwasilisha shairi “Bathidei Jambo Jambo”, ambalo lilielezea changamoto zinazoibuka mzazi anapothamani mtoto mmoja zaidi ya wengine. Mafunzo yake ni kuwa watoto wanastahili kukuzwa kwa njia sawa bila kujali jinsia ama uwezo.

Wasichana wa Mwaani Girls na Mwalimu wao Joan Muchina wakionesha nakala za filamu ya ‘Juda’ waliyotayarisha. Picha/ Anthony Njagi

Nao mchezo wa shule maalum ya Gianchere kutoka eneo la Nyanza ilikuwa na mchezo “Mercy Angel”. Mercy ni yatima ambaye anakandamizwa na shangazi yake, kabla ya kupata msamaria mwema ambaye anamuokoa na kuhakikisha kuwa anafaulu katika talanta yake ya kucheza densi.

Baadhi ya Shule nyingine zilizoshiriki jana ni Word of Life Christian Academy Mombasa, Chogoria Boys Boarding , ACK Holy Trinity Academy,  Kericho, Rift Valley, St Andrews Kabare na Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi.

Chuo Kikuu cha Kisii kilikuwa na mchezo ‘In my book’, ambao unaelezea jinsi sanaa haijathaminiwa, na wengi wanazingatia kuwekeza katika teknolojia na mashini, hali ambayo inaonekana kuzorotesha zaidi maadili katika jamii.

Wasichana wa Mwaani Girls na Mwalimu wao Joan Muchina wakionesha nakala za filamu ya ‘Juda’ waliyotayarisha. Picha/ Anthony Njagi

Katika mchezo huo,  Oliver (ambayo inaigizwa na Fred) anapitia shida nyingi kujaribu kumshawishi babake Prof Abednego (inayoigizwa na Curtis) na wawekezaji kufikiria kuwekeza kwa sanaa ambayo ni muhimu kukuza maadili yanayoongoza teknolojia.

Prof  Prof Akama na chuo cha Kisii wanaamini kuwa iwapo usanii utapewa nafasi, sio tu kukuza ubunifu bali kutoa nafasi kwa vijana, kuelimisha jami, lakini pia kwa njia kubwa kuunda jinsi binadamu anaweza kuishi kwa uwiiano miongoni mwa jamii.