Habari MsetoSiasa

Mwafaka uliua nguvu za NASA, asema Mudavadi

July 10th, 2018 2 min read

Na RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC) amekiri kuwa muafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga umeathiri uwezo wa upinzani kutekeleza majukumu yake ya kukosoa serikali.

Sasa ametoa wito kwa makanisa kujitokeza kwa ukakamavu zaidi kuzungumzia ufisadi na masuala mengine yanayokumba nchi.

Bw Mudavadi alisema viongozi wengi wa upinzani na wengine wa Jubilee wanaogopa kuzungumza kuhusu maovu yanayoendelea serikalini kwa kuhofia kwamba wataadhibiwa kwa kutounga mkono muafaka wa viongozi hao wawili.

Ingawa viongozi kadhaa wanaamini muafaka huo umesaidia kutuliza taharuki ya kisiasa nchini, Bw Mudavadi alisema viongozi hawajitahidi kuchunguza sakata za ufisadi zinazochipuka nchini.

“Lazima nikiri kwamba upande wa upinzani umedunishwa. Hauna nguvu kama ilivyokuwa awali,” akasema baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa la Jesus Celebration Center, Kisumu.

Aliongeza kuwa inahitajika kuwe na upande thabiti wa upinzani kwani wale walio katika Muungano wa NASA sasa wanajiepusha kukashifu wakuu serikalini.

“Huwa tunashirikiana na serikali kwa masuala mengi lakini hilo halifai kuwa sababu ya kuangamiza upinzani,” akasema Bw Mudavadi.

Hata hivyo, aliongeza kuwa kutakuwa na upinzani wenye nguvu zaidi ambao utasikika katika siku chache zijazo.

Awali upande wa upinzani ukiongozwa na Bw Odinga ulikuwa ukisikika sana kila wakati ambapo mambi yalikuwa yakienda mrama serikalini.

Msimamo ambao ungechukuliwa na Bw Odinga pamoja na vinara wenzake katika NASA akiwemo Bw Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya), ungefuatwa na viongozi waliochaguliwa kupitia kwa vyama hivyo na kufanya serikali kujirekebisha.

Bw Mudavadi alisema vitengo vya uongozi ikiwemo bunge havijaridhisha Wakenya hasa baada ya kamati ya bunge kutoa ripoti duni kuhusu sukari ya magendo wiki iliyopita.

Kiongozi huyo wa ANC alijiunga na viongozi wengine waliodai kwamba uchunguzi huo wa kamati ya pamoja ya biashara na kilimo bungeni haikutekeleza wajibu wake ilivyotarajiwa na wananchi.

“Sauti ya wanasiasa inakanganya na kutuma mchanganyiko wa ujumbe kwa umma. Tunahitaji kanisa liingilie kati na lihakikishe serikali inatekeleza majumu yake ipasavyo,” akasema.

Maoni yake yaliungwa mkono na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Vihiga, Bi Beatrice Adagala, na Mbunge wa Butere, Bw Tindi Mwale, ambao walisema watatumia mamlaka yao bungeni kuhakikisha maovu ya serikali yanafichuliwa na kukashifiwa ipasavyo.

“Hatufai tuwe tunachekeshana na mashahidi au washukiwa waliohusishwa na ufisadi. Kama wabunge, inafaa tuchunguze kwa kina zaidi na kuhakikisha tunaambia umma kile kinachoendelea,” akasema Bw Mwale.

Viongozi wa eneo la Magharibi walireelea wito wao kumtaka Rais Kenyatta aunde jopo la kuchunguza biashara ya sukari ya magendo nchini na kusaidia kufufua viwanda vilivyofilisika vya kutengeneza sukari.

Wanataka jopo hilo lisimamiwe na jaji wa Mahakama ya Juu.