Habari

Mwafrika kuwa mkuu wa ISO kwa mara ya kwanza kabisa

September 17th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

KWA mara ya kwanza kwa muda wa miaka 70, Mwafrika atakuwa mkuu wa Shirika la Viwango vya Ubora vya Kimataifa (ISO).

Bw Eddy Njoroge, ambaye pia ni mwanakamati wa Shirika la Viwango vya Ubora Nchini (Kebs) na mwenyekiti wa zamani wa Nairobi Securities Exchange, anatarajiwa kuthibitishwa kama Rais wa kwanza Mwafrika katika Mkutano wa Baraza Kuu la ISO ambalo limeanza mjini Capetown, Afrika Kusini.

Bw Njoroge (66) ambaye aliambulia patupu mnamo mwaka 2016 alipojaribu kwa mara ya kwanza, ana uzoevu wa zaidi ya miaka 10 katika sekta hiyo.

Pia, aliweka historia kwa kuifanya kampuni ya Kenya Electricity Generation Company (KenGen) kuwa kampuni ya kwanza ya umma kufikia kiwango cha ISO 9001 mnamo mwaka 2004.

“Nitaweka ahadi yangu niliyotoa nilipochaguliwa kuwa nitahakikisha viwango vya bidhaa na huduma zinaafikiana na zile za kimataifa ili kuhakikisha ubora,” akasema Bw Njoroge.

Viwango vya ISO husaidia katika kupenya katika soko la kimataifa na hufafanua viwango ambavyo huduma na bidhaa zinafaa kufuatilia na kufikia ili kusafirishwa nchi zingine.

Wakati wa uongozi wake, Bw Njoroge atafanya kazi jijini Nairobi ambapo anachukua nafasi ya Bw John Walter wa kutoka Canada.